Featured

    Featured Posts

KAMATI KUU YAJADILI TAARIFA ZA CAG NA TAKUKURU, YAIELEKEZA SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WALIOSABABISHA UBADHIRIFU

Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeielekeza Serikali kuchukua hatua thabiti kwa waliobainika kuhusika katika ukiukaji wa sheria na kusababisha ubadhirifu wa mali na rasilimali za nchi.

Imetoa maelekezo hayo baada ya kupokea na kujadili kwa kina masuala mbalimbali ya kitaifa, ikiwemo Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taarifa ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kwa mwaka wa fedha 2021/22, zilizowasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan, hivi karibuni.

Akizungumza baada ya Kikao cha Kamati Kuu hiyo kilichofanyika leo, Ikulu Jijini Dar es Salaam, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Sophia Mjema, amesema katika kuzijadili taarifa hizo Kamati Kuu imebaini kuwepo maeneo ambayo taarifa zote zimeonesha kuwa Serikali imeboresha na kuendelea kuimarisha kasi ya utoaji wa huduma kwa wananchi, ikiwemo udhibiti na umakini katika matumizi ya fedha za umma, ambapo katika taasisi zilizokaguliwa, asilimia 96 zimepata hati safi.

Amesema, katika mjadala huo wa kina Kamati Kuu imesikitishwa na kuwepo baadhi ya maeneo mengine ambayo bado yanatakiwa kufanyiwa kazi ili kuondoa mapungufu au udhaifu uliobainishwa, ikiwemo mifumo ya malipo na ukusanyaji wa mapato kutokusomana.

Pia imesikitishwa, kuwepo kwa baadhi ya watumishi wa umma wasiokuwa waadilifu, hali inayosababisha serikali kukosa mapato na kupata hasara, uwepo wa mashirika ya umma yanayojiendesha kwa hasara na vitendo vya ubadhirifu wa mali na rasilimali za umma, kama vile kuongeza bei za manunuzi ya Serikali.

Mwenezi Mjema amesema, katika maazimio Kamati Kuu imeipongeza Ofisi ya CAG na ya TAKUKURU, kwa kufanya kazi zao kwa weledi na kuendelea kutimiza wajibu wao kwa taifa, kwa kuonesha maeneo ambayo Serikali imeyaboresha na kubainisha madhaifu yanayohitaji kufanyiwa kazi, kwa lengo la kulinda mali, rasilimali kwa maslahi ya taifa.
 
Pia Kamati Kuu imetoa maelekezo kwa Serikali kuwafuatilia watu wote wanaotumia dhamana za uongozi vibaya na kushindwa kuweka maslahi ya nchi na uzalendo mbele katika nafasi walizoaminiwa kutumikia watu, badala yake wanaweka maslahi binafsi.

Amesema pia Kamati Kuu imezipongeza Serikali zote mbili za CCM, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Rais Samia na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Rais Hussen Ali Mwinyi kwa kuendelea kutekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2020 – 2025 kwa vitendo, kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa Watanzania wote.

Kuhusu ziara ya siku tatu iliyofanywa na Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris, Mwenezi Mjema amesema Kamati Kuu ya CCM, imeipongeza Serikali kwa kuratibu na kufanikisha vema ziara hiyo na kwamba imeongeza uimara wa ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani na kufungua milango zaidi ya mahusiano yenye faida kwa maendeleo na ustawi kwa pande zote mbili, hususan katika maeneo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, kukabiliana na magonjwa, uchumi, uwekezaji na ajira.

 

Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Sophia Mjema akizungumza na waandishi wa habari leo Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana