Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt Doto Mashaka Biteko amelipongeza Shirika la umeme Tanzania -TANESCO usimamizi makini na hatua kubwa iliyofikiwa kwenye ujenzi wa mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere, ambao mpaka sasa umefikia asilimia 91.72.
Dkt Biteko amesema hayo leo alipofanya ziara ya kutembelea mradi wa Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere, lililopo Rufiji Mkoani Pwani.
Naibu Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, imefanya kazi kubwa ya kusimamia kwa karibu mradi huu, hivyo watanzania wanakila sababu ya kuwa na imani na TANESCO.
Aidha amesema lengo kubwa la Serikali ni kutaka watanzania wapate umeme wa uhakika ambapo suluhisho mojawapo ni kukamilika kwa mradi wa JNHPP.
Mradi wa bwawa la kufua umeme wa Julius Nyerere ulianza ujenzi wake Desemba 12, mwaka 2018 na unagharimu kiasi cha shilingi Trilioni 6.5 na hadi sasa mkandarasi amekwishalipwa kiasi cha shilingi trilioni 5.6 cha malipo yote.
Ziara hiyo inakuwa ya kwanza kufanywa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati mpya ambaye ni Doto Biteko tangu ateuliwe cheo hicho na Rais Dkt Samia hivi karibuni.
Naibu Waziri Mkuu Biteko akipewa maelezo na Mhandisi KitendoI Mwandambo, ambaye ni Mhandisi Mkazi Mradi wa Bwawa la kufua Umeme la Julius Nyerere wakati wa ziara hiyo.
Post a Comment