Na Lydia Lugakila,
Mkuu wa Wilaya ya Misenyi Mkoani Kagera Kanali Wilson Sakulo ameitaka tume iliyoundwa kufuatilia masuala ya ushoga na ulawiti katika shule zote za Wilaya ya Misenyi kuhakikisha inakamilisha ufuatiliaji mara moja ili kuona ni kwa kiasi gani suala limewaathiri vijana hao.
Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani cha robo ya kwanza, 2023/2024 cha siku ya pili kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo Oktoba 27,2023 Kanali Sakulo amesema kuwa kumekuwa na changamoto kubwa hasa katika upande wa malezi ya vijana ambapo katika baadhi ya shule za Wilaya hiyo kuna vitendo vya ulawiti na ushoga vinaendelea kimya kimya.
"Kwakweli inatisha unaweza usiamini ila mambo hayo yanafanyika, nilishatoa maelekezo kwa tume iliyopewa kazi ya kuhakikisha ufuatiliaji unafanyika katika shule zote hivyo uharaka ni lazima uwepo ili kuwanusuru vijana wetu" alisema Kanali Wilson Sakulo.
Ameongeza kuwa unakuta Mwalimu anamlawiti Mwanafunzi, Mwalimu anatembea na Mwanafunzi, Mwalimu anawageuza Wanafunzi mashoga na kuwa hivyo ni vitu vya ajabu sana na vinapaswa kukemewa haraka.
Aidha amewaomba Wazazi kufuatilia watoto wao kwani changamoto hiyo imekuwa kubwa.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya ya Misenyi amewahimiza madiwani katika Halmashauri hiyo kusimamia kwa karibu pamoja na kukagua miradi mbali mbali ya maendeleo kutokana na miradi mingi kuletwa katika maeneo yao.
"Nimpongeze Rais Samia kwa jinsi alivyoipendelea Wilaya yetu miradi ni mingi na katika hilo madiwani niwaombe tuiongelee miradi hiyo iletwayo na Rais wetu tuhakikishe Wananchi wanajua Serikali yao imeleta kiasi gani ikiwa ni pamoja na miradi inayoendelea iwekwe wazi.
Akizungumzia suala la ukusanyaji wa mapato alisema Halmashauri hiyo imezidi kufanya vizuri ambapo mwaka 2022/2023 makadirio ilikuwa wakusanye sh. Bilioni 4 lakini walifanikiwa kukusanya hadi Sh Bilioni 6 jambo lililomfanya kuwapongeza wataalam mbali mbali na Madiwani kwa kazi hiyo.
Hata hivyo kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi Projestus Tegamaisho amesema kuwa kutokana na Serikali kuwaagiza kwamba ifike hatua Halmashauri zijitegemee hivyo wataalam na Madiwani wataendelea kubuni vyanzo vya mapato, kuboresha baadhi ya vyanzo ili viwe vya kisasa pamoja na kuanzisha vipya ili mapato yaongezeke zaidi.
Post a Comment