Baadhi ya maagizo ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM, Komredi Daniel Chongolo aliyoyatoa hivi karibuni wakati wa ziara yake katika mikoa ya Katavi na Rukwa yameanza kutekelezwa, ambapo tayari Wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) wakiongozwa na Mwenyekiti Anthony Dialo wametua mkoani Katavi kutafutia ufumbuzi wa changamoto ya Mbolea.
Akizungumzia kuhusu ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dialo amesema kuwa ina lengo la kujifunza namna tasnia ya mbolea inavyosimamiwa, kusikiliza na kutafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wadau wa tasnia ya mbolea nchini.
"Bodi hii ni mpya hivyo tumeona kuliko kutegemea taarifa zinazotolewa na menejimenti ni vyema tukawatembelea na kuwasikiliza wadau wetu ili tunapojadili mada tuwe na uelewa wa yale yanayotendeka katika maeneo mbalimbali nchini" Dkt. Diallo alisema.
Imedhihirisha wazi kwamba ziara hiyo ni mwitikio wa wa maagizo ya Komredi Chongolo aliyoitaka Taasisi hiyo kwenda katika mikoa hiyo, kupitia na kuhakikisha wakulima wanapata mbolea ya ruzuku mapema kabla ya msimu kuanza na waipate katika maeneo ya karibu, tofauti na msimu uliopita ambapo kulikuwa na malalamiko ya wananchi kuwa mbolea hiyo ilichelewa kufika na walilazimika kuifuata umbali mrefu kuipata.
Akizungumza wakati wa kikao baina ya wajumbe wa bodi hiyo na Uongozi wa Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwamvua Hoza Mrindoko ameiomba mamlaka kufikisha elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kutokana na imani ya wananchi wa mkoa huo kuwa ardhi yao inarutuba.
Aidha, ameishukuru Bodi hiyo kwa kuona umuhimu wa kuwatembelea na kupokea maoni na changamoto wanazokutana nazo wakati wakitekeleza majukumu yao kwa wananchi.
Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Mkoa wa Katavi, Faridu Mtiru akiwasilisha taarifa ya Mkoa, amesema changamoto wanayokutana nayo ni uchache wa Mawakala wa mbolea na kueleza waliosajiliwa ni mawakala 25 lakini wanaofanya kazi ni 10 pekee na kuiomba Mamlaka kuongeza idadi ya mawakala ili kuwafikia wakulima karibu na maeneo yao.
Akieleza juhudi za Mamlaka katika kutatua changamoto ya uchache wa mawakala, Meneja wa TFRA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Michael Sanga amesema changamoto hiyo imetafutiwa ufumbuzi kwa kushirikisha vyama vya ushirika na tayari mafunzo yamekwisha tolewa utekelezaji utaanza punje.
Ziara hiyo imelenga kutembelea mikoa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mkoa wa Katavi.
Post a Comment