Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri akizungumza alipokuwa akifungua kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule warsha kuhusu dhana ya wamiliki manufaa wa kampuni na majina ya biashara jijini Dodoma Desemba 5, 2023.
Waliohudhuria semina hiyo ni; mawakili, wahasibu, wafanyabiashara na maafisa kutoka kampuni za ushauri wa biashara mkoani humo.
Mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Makampuni wa wakala hiyo, Harvey Kombe akielezea umuhimu wa warsha hiyov kwa wadau hao pamoja na kuwaeleza marekebisho ya baadhi ya sheria za usajili wa biashara na kampuni.Afisa Habari wa BRELA, Glory Mbilimonyo akisema maneno ya utangulizi wakati wa warsha hiyo.
Afisa Habari wa Brela, Jacob Mkuye akiwasilisha mada kuhusu dhana ya wamiliki manufaa wa kampuni.
Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Kanda ya Dodoma (TLS), Wakili Mary Munissi akielezea jinsi washiriki watakavyonufaika na warsha hiyo pamoja na kuipongeza BRELA kuwaandalia.
Afisa wa BRELA, Edward Magahyane akiwasilisha mada ya dhana ya wamiliki manufaa wa majina na biashara.
Baadhi ya washiriki wakiwa katika warsha hiyo.
DC Shekimweri akipongezwa na Wakili Munissi baada ya kufungua warsha hiyo.
DC Shekimweri akiondoka baada ya kufungua warsha hiyo
Na Richard Mwaikenda, Dodoma
WAFANYABIASHARA wametakiwa kuacha tabia ya kufanya biashara kiujanja ujanja kwa kutosajili majina ya biashara na kampuni zao na kukwepa kulipa kodi wakidhani wananufaika bila kujua kwamba wanakosa fursa mbalimbali za maendeleo ikiwemo mikopo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alipokuwa akifungua Warsha kuhusu dhana ya umiliki manufaa wa kampuni na majina ya biashara iliyohudhuriwa na mawakili, wahasibu, kampuni za ushauri wa maendeleo ya biashara na wafanyabiashara iliyoandaliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) jijini Dodoma Desemba 5, 2023.
"Kutokulipa kodi, kutokusajili kampuni kutokuwa na leseni, kufanya biashara kienyeji, au kwa janja janja, unaweza ukaona ni ujanja lakini mwisho wa siku huwezi ukafanikiwa, itakunyima fursa ya kukopa, utakuwa na mapato makubwa mkononi lakini ukija kwenye nyaraka, taarifa na kumbukumbu na rekodi za ulipaji wako wa kodi utakuwa umedanganya kwa hiyo huwezi kupata mkopo na kubaki kuwa mlalamishi kuwa hupewi mkopo,"amesema Shekimweri.
Shekimweri ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amewahimiza wafanyabiashara kufanya biashara katika mazingira rasmi kwa lengo la kupata mafanikio. "Hakuna anayefanya biashara kwa kutegemea mtaji uleule halafu aendelee, mfanyabiashara huyo hayupo,"amesisitiza.
Amewataka washiriki hao kutumia mafunzo hayo yaliyotolewa na BRELA ili wajifunze Sheria na Kanuni za umiliki manufaa katika kampuni na utaratibu wa kuwasilisha taarifa kwa msajili wa kampuni.
Naye Mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, ambaye ni Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Makampuni wa wakala hiyo, Bw. Harvey Kombe amesema kuwa taasisi hiyo imeonesha nia ya kuendelea kukutana na wadau kwa lengo la kushauriana na kuelekezana kuhusiana na mabadiliko ya sheria mbalimbali pamoja na fursa ya kuwasikiliza wadau na kuelezea walichowaandalia kutokana na shughuli wanazozifanya kila wakati, ikiwemo marekebisho ya Sheria ya makampuni Sura namba 212 ya upatikanaji wa taarifa za umiliki manufaa.
Aidha, ametaja Sheria ya ya mwaka 2022 ya marekebisho ya majina ya biashara Sura 213 iliyowekwa takwa kwa wamiliki biashara na ubia kutoa taarifa za umiliki manufaa kwa msajili wa majina, biashara na kampuni na kwamba mabadiliko hayo yameenda sambamba kwa Waziri wa Viwanda na Biashara kutunga kanuni ambazo tayari zimepitishwa na kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mawakili Kanda ya Kati Dodoma, Wakili Mary Munissi ameungana na kauli ya Mkuu wa Wilaya Dodoma, Shekimweri kwa kuwataka wateja wao kujenga tabia ya kufuata sheria na kanuni za biashara za kusajili kampuni zao na kulipa kodi kwa mujibu wa sheria.
Ametoa wito kwa mawakili kuacha tabia ya kuwakumbatia kwa kuwatetea wateja wao wanaokiuka taratibu, sheria na kanuni hizo, bali kinachotakiwa ni kuwaelimisha umuhimu wa kuzifuata bila shuruti.

Post a Comment