Na Mwandishi Maalum, Dar es Salaam
Kwa mara ya pili mfululizo, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) CPA. Hosea Kashimba, ameibuka kidedea kwa kuwa mshindi wa kwanza katika kundi la watendaji wakuu wa Taasis za Umma mwaka 2023.
Mwaka jana, 2022 CPA. Kashimba alijishindia tuzo hiyo pia. Kwa kushinda tuzo kwa mwaka huu, inaonesha wazi kuwa Mkurugenzi Mkuu huyo wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) yupo makini katika utendaji wake. Pamoja na CPA. Kashimba, wakurugenzi wengine wa PSSSF wameongoza katika makundi yao.
Wakurugenzi hao ni Mkurugenzi wa Fedha PSSSF, Bi. Beatrice Musa-Lupi, ambaye ameshinda tuzo ya Mkurugenzi wa fedha wa mwaka, Bw. Mbaruku Magawa, ambaye amekuwa mshindi wa tuzo ya Mkurugenzi Uendeshaji wa Mwaka na Bw. Gilbert Chawe, Mkurugenzi wa TEHAMA, ambaye yeye amekuwa miongoni mwa washindi wa tuzo ya Ubunifu na Teknolojia.
Tuzo hizo za umahiri wa uongozi zinazotambulika kama The Top 100 Executive List 2023 Awards zimetolewa jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki.
Akiongea katika tafrija ya kukabidhi tuzo hizo, Mgeni Maalum Thamsanqa Maqubela, kutoka taasisi ya Global CEO Institute ya Jamhuri ya Afrika Kusini; aliwaasa vingozi waliokabidhiwa tuzo kuendelea kuimarisha mbinu zao za kiuongozi ili kuleta tija na ufanisi.
Aidha aliwahakikishia kuwa Tanzania ina fursa nyingi za ukuaji wa haraka wa kiuchumi na kwa kuzingatia fursa za kibiashara zilizopo sasa Afrika; basi matarajio ni kuimarika kwa soko la hisa la Dar es Salaam (DSE).
Tuzo hizi zinaratibiwa na waratibu wa Top 100 Executive Tanzania na Global CEO Institute ya Jamhuri ya Afrika Kusini ili kutambua viongozi 100 mahiri kila mwaka kwa kutathmini utendaji, umahiri, ustadi, ubora na uwezo.
Tuzo hizi ni kielelezo cha umahiri na ukuaji wa taasisi katika kuonesha ukuaji wa faida, ukuaji kifedha, ubunifu na huduma.
CPA. Kashimba, akibadilishana mawazo na Mkurugezni Mtendaji wa ATCL, Bw.Ladislaus Matindi.
Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, PSSSF, Bw. James Mlowe (katikati) akifurahia ushindi huo na timu yake, Afisa Mkuu wa Uhusiano, Bi. Fatma Elhady (kushoto) na Afisa Uhusiano Mwandamizi, Bi. Coleta Mnyamani.




Post a Comment