Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu( wa pili kulia) akiangalia na huku akipewa maelezo na Afisa Misitu, John Mtika kuhusu hatua za miche ya miti ya miembe inavyokua wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea ofisi za Kurugenzi ya Uzalishaji miche ya Miti mkoani Morogoro kwa lengo la kujua imejipangaje kuzalisha miche za miti yenye ubora ikiwemo ya mbao pamoja na ya matunda ambayo itasambazwa nchi nzima Kulia ni Mkurugenzi wa Kurugenzi hiyo, Edgar Masunga pamoja na watumishi wengine.
--------------------
NA LUSUNGU HELELA-MOROGORO
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu ameahidi kulifanyia kazi suala la kugawa miche ya miti bure kwa Wananchi ili wakaipande iliyooteshwa na Kurugenzi ya Uzalishaji miche ya miti kuwa utaratibu huo hauwezi kuleta matokeo yaliyokusudiwa na Serikali.Imeelezwa kuwa uzoefu uliopo unaonesha kuwa vitu vingi ambavyo Serikali imekuwa ikivigawa bure kwa Wananchi bila wananchi hao kuchangia gharama yoyote vitu hivyo hushindwa kuthaminiwa.
Mhe. Kanyasu alitoa kauli hiyo jana mkoani Morogoro wakati alipotembelea ofisi za Kurugenzi hiyo kwa lengo la kujua imejipangaje kuzalisha miche za miti yenye ubora ikiwemo ya mbao pamoja na ya matunda ambayo itasambazwa nchi nzima.
Alisema utaratibu huo itabidi uangaliwe upya kwa vile ni ngumu kwa wananchi walio wengi kuitunza kwa sababu hawasikii uchungu na walio wengi hujikuta wakiitupa au kuiacha bila kuimwagilia hadi inakufa.
''Ukichukua miche leo halafu ukaipeleka mkoani Shinyanga ukagawa bure yote italiwa na ng'ombe na vivyo hivyo ukaipeleka Dodoma yote itakufa kwa vile haitamwagiliwa maji kwa sababu ni ya bure'' Amesisitiza
Alisema siku zote kitu cha bure hakithaminiwi, hivyo lazima kila Mwananchi achangie kidogo lakini isiwe bure kabisa.
Hata hivyo, Mhe. Kanyasu alisema miche ya miti inaweza kutolewa bure kwa taasisi za umma kama vile shule ila kwa makubaliano maalumu lakini sio kwa wananchi.
Aidha, Aliitaka Kurugenzi hiyo ijiendeshe kibiashara badala ya kujikita kutoa huduma kwa wananchi
Katika hatua nyingine, Mhe Kanyasu aliiagiza Kurugenzi hiyo ifungue utalii wa bustani wa miti na maua katika jiji la Dodoma ambao ni moja ya aina ya utalii unaopendwa sana hasa na Wanamazingira.
Alisema miji kama Arusha pamoja na Mwanza imeanzisha utalii huo licha ya kuwa kumekosekana mwongozo wa kuziboresha bustani hizo lakini hata hivyo watalii wengi wamekuwa wakimiminika katika bustani hizo.
Post a Comment