 |
Na Debora Sanja, Bunge
Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai amewataka watumishi wa Bunge kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake wafanya kazi kwa bidii.
Mhe. Spika alitoa rai hiyo kupitia hotuba yake iliyosomwa na Naibu Spika, Mhe. Dkt. Tulia Ackson katika uzinduzi wa Baraza la Wafanyazi la Ofisi ya Bunge lililofanyika katika Ofisi Ndogo za Bunge Tunguu Zanzibar.
Alisema kunahitajika mabadiliko katika kutelekeza majukumu ya kila siku kwa watumishi kuchapa kazi kwa bidii ili kueleta utendaji wenye tija na ufanisi.
Aliwataka wajumbe kupitia mada zitakazowasilishwa katika Mkutano huo wa Baraza kukumbuka wajibu wao katika kutelekeza majukumu waliyopewa kulingana na taaluma husika na hatimaye kufanikisha utekelezaji bora wa majukumu na madaraka ya Bunge Kikatiba.
Aidha, alimpongeza Katibu wa Bunge, Ndugu Stephen Kagaigai kwa kufanikisha utatuzi wa changamoto za muundo wa Ofisi ya Bunge ambao umewezeshwa kuundwa kwa Baraza la Wafanyakazi.
“Naomba nitumie fursa hii kuwapongeza watumishi wote mlioteuliwa na Tume ya Utumishi wa Bunge kushika nyadhfa mbalimbali za uongozi na nimatumini yangu kwamba mtatumia uwezo na karama mlizojaaliwa na Mwenyezi Mungu katika kutekeleza majukumu yenu kwa ufanisi na kuliwezesha Bunge kufikia malengo yake,” alisema.
Aliwapongeza pia wajumbe na wawakilishi wa Idara na Vitengo kwa kuchaguliwa kushika nafasi hiyo na kuwataka kuitumia nafasi hiyo kuwa kiungo kati ya Wafanyakazi wa kada na ngazi zote, Menejimenti na Tume ya Utumishi wa Bunge.
Awali akizungumza katika mkutano huo, Katibu wa Bunge Ndugu Stephen Kagaigai alisema Ofisi ya Bunge imeunda Baraza la Wafanyakazi baada ya Baraza hilo kutokuwepo katika kipindi kirefu kutokana na changamoto za kimuundo zilizokuwepo.
Alisema lengo la Baraza hilo lililopo kisheria ni kuboresha utendaji kazi wa taasisi kwa kufanya kazi kwa ushirikiano na siyo ugomvi na mifarakano.
Kabla ya uzinduzi wa Baraza hilo, wajumbe walimchagua Ndugu Frank Mbilinyi kuwa katibu wa Baraza na Ndugu Felister Njovu kuwa Katibu Msaidizi.
|
Author Name
Author Description!
Get Free Email Updates to your Inbox!
Post a Comment