Uchunguzi uliofanywa na kanali ya televisheni ya CNN umebaini kuwa, silaha za Marekani zilizonunuliwa na muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia katika mashambulizi yake dhidi ya Yemen ziko mikononi mwa magenge yenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda na makundi mengine ya Kisalafi yenye misimamo ya kufurutu ada nchini Yemen.
Upekuzi uliofanywa na CNN umefichua kuwa, silaha hizo za kijeshi za Marekani zimekabidhiwa magenge ya kigaidi na waasi nchini Yemen, huku zingine zikiishia mikononi mwa kundi linalotaka kujitenga la kusini mwa Yemen, linalougwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Aidha silaha hizo zilizotengenezwa Marekani zinamilikiwa na makundi yenye kumuunga mkono Abd Rabbuh Mansur Hadi, rais mtoro wa Yemen aliyekimbilia Saudi Arabia baada ya kujiuzulu.
Seneta Elizabeth Warren wa Massachusetts na pia mgombea wa urais kwa tiketi ya chama cha Democratic katika uchaguzi ujao nchini Marekani ameapa kufuatilia yaliyomo kwenye uchunguzi huo wa CNN, huku akiushutumu utawala wa Donald Trump kwa kukanyaga sheria za mauzo ya silala.
Serikali ya Donald Trump inapinga hatua yoyote ya kubana au kutaka kusitisha mahusiano yake ya kijeshi, kisilaha na kilojistiki na watawala wa kifalme wa Saudi Arabia.
Tarehe 17 Aprili mwaka huu Trump alipigia veto azimio la Kongresi ya Marekani lililotaka kusitishwa himaya na misaada ya kijeshi ya Washington kwa Saudia na washirika wake katika vita vya Yemen.
Post a Comment