Featured

    Featured Posts

MIAKA 20 BILA BABA WA TAIFA NA MSAMAHA WA WAHUJUMU UCHUMI WA RAIS MAGUFULI


Judith Mhina-Maelezo

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni kati ya Marais wachache duniani ambao walikuwa  na utaratibu wa kusamehe watu wanaomkosea binafsi  na Taifa, kama vile wahujumu uchumi  na wahaini ambao walikuwa na fikra za kupata madaraka isivyo halali.

Baba wa Taifa tunamkumbuka  kwa matendo yake yaliyotukuka ambayo ni darasa tosha kwa viongozi hapa Tanzania na duniani kwa ujumla hususan Barani Afrika. Wapo viongozi wengi na wana zuoni ambao hawalali usiku na mchana kuchimba fikra za Mwalimu Nyerere na kuhimiza zifuatwe na kutekelezwa kwa kuwa zilikuwa na lengo la kuwaendeleza Waafrika na zina tija mpaka sasa.

Kati ya matendo hayo ni pale Mwalimu Nyerere anapowasamehe  watu mbalimbali walliomkosea hata kama sheria ilielekeza wafungwe maisha, kunyongwa hadi kufa  na adhabu nyinginezo lakini binafsi dhamira yake ilimtuma kuongea nao na kuwasamehe.

Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli alitoa ushauri wakati akiwaapisha baadhi ya viongozi uliowateua tarehe 22 Septemba 2019, kuhusiana na watuhumiwa ambao wako tayari kukiri na kukubali kurejesha fedha za Watanzania katika kesi za madai za uhujumu uchumi.

“Rais Magufuli amesema siwezi kuongoza Taifa la watu wenye machozi, hivyo natoa rai wale wote ambao wapo mahabusu kwa tuhuma ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha nashauri  waandike barua ya kuomba radhi na kukiri makosa ili warejeshe fedha za umma walizochukua ili zikajenge shule, hospitali barabara na masuala mengine ya maendeleo”

Akimuelezea Rais Magufuli juu ya walioandika barua ya kuomba msamaha na kukiri makosa Muendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali Biswalo Mganga amesema jumla ya watuhumiwa 467 wenye kesi za uhujumu uchumi wameandika barua na kuomba kukiri makosa yao. 

“Kati ya hao waliokiri, jumla ya shilingi Bilioni saba mia nane themanini na nne elfu mia tisa na moja na mia tano ishirini na sita (7,884, 901, 526) fedha za Tanzania, wako tayari kurudisha muda wowote kuanzia sasa”.

Aidha, kwa wale ambao walichukua fedha za kigeni ni jumla ya Dola za Amerika, elfu mbili mia tano sitini na tatu elfu, mia saba na nne na senti hamsini na nane,( 2, 563,704.58)  sawa na fedha za Tanzania Bilioni  tano milioni mia saba kumi na saba elfu sitini na moja na mia tatu na kumi na nne. (5, 717, 061, 314) zinarejeshwa alisema Mganga.

Watanzania waliowengi wanaona ni maajabu na ni kitu kisichewezekana katika dunia hii lakini la hasha, hata Baba  wa Taifa Mwalimu Nyerere wakati wa vita vya uhujumu uchumi mwaka 1982-1984 watuhumiwa  wa Uhujumu uchumi  walitupa bidhaa mali na vitu kadhaa kwa kuhofia kukamatwa.

Aidha, wahujumu uchumi walio wengi walikamatwa na kukiri makosa yao na kuahidi hawataficha bidhaa, mali na vitu vinavyohitajika katika maisha ya kila siku ya Mtanzania au kuuza kwa bei ya juu (wakatu ule bei ya kuruka) ili kuihujumu serikali ya Tanzania. Lengo likiwa kuifanya Tanzania ikosolewe Kimataifa na kumpaka matope Baba  wa Taifa ambaye alikuwa na heshima ya kipekee duniani aonekani hafai. 

Hivyo, sio ajabu kwa Rais Dkt Magufuli kuhujumiwa na kulaumiwa kwa mema anayoyafanya na wasioitakia mema nchi yetu. Eti analaumiwa kwa kitendo chake cha kushauri na kuwapa nafasi wahujumu uchumi kukiri makosa yao na kurejesha fedha za Watanzania, ni ukweli usiopingika watu wanaokosoa  msamaha huu wanafanya hivyo kwa masilahi  yao binafsi.

Akiwasilisha kundi la pili ambalo lipo tayari kulipa fedha walizochukua kwa awamu Biswalo Mganga  amesema “Jumla ni Bilioni tisini na nne mia mbili arobaini mia moja hamsini elfu na tano elfu  watarejesha kwa awamu  (94,240, 155, 000) na kufanya jumla kuu ya fedha zote ambazo wahujumu uchumi walioomba na ambao wako tayari kuzirudisha ni Bilioni 107,842,112,744: 04”

Hii , ikiwa ni pamoja na mdaiwa wa Dola za Amerika laki nne na nusu (4,500) ambazo mtuhumiwa  alikuwa mahakamani ijumaa tarehe 27 Sept, 2019 na kukubali kuitikia wito wa kukiri na kurejesha fedha. Ambazo zina dhamani ya fedha za Tanzania Bilioni moja thelathini  na sita elfu mia sita sabini na mbili milioni (Bilioni  1, 036, 672, 000) ambazo zimelipwa pamoja na faini ya milioni tano zaidi. Alimalizia Biswalo Mganga.

Huu ni ujasiri  na utayari wa Watanzania wanapotenda kosa na kuonekana kihalali kweli wamelitenda wanapewa nafasi ya kukiri na kurejesha walichochukua. Hii yote inafanyika kwa masilahi ya Watanzania kwa kuwa hata kama akifungwa haitakuwa na mantiki kwa kuwa fedha ambazo zingewaletea maendeleo Watanzania hazitarudi.

Matendo yote haya yanaiwekea Tanzania katika ramani ya dunia  kuwa nchi ya Amani, Upendo na Mshikamano kwa kuwa kila mmoja anapewa nafasi ya kuongea kukiri na kurejeshwa katika jamii. Hii ina maana kubwa jamii inakuwa radhi  na ndio matokeo ya sasa kila Mtanzania kuona fahari kulipa kodi, ambayo inawanufaisha watu wote.

Tukubali  funzo hili tunalolipata kutokana na zoezi zima la Watuhumiwa kukaa ndani kwa siku kadhaa, na kuona adha waliyoipata wakiwa mahabusu, pamoja na kuishia kurejesha kile ambacho walidhani wana uhalali wa kuwadhulumu Watanzania. Hali hii italeta nidhamu ya fedha na mali za serikali kutochezewa hovyo na kudhani itawanufaisha Wahujumu uchumi na familia zao. 

Bado Rais Magufuli alitoa tahadhari kwa kuongeza siku saba za msamaha na baada ya hapo wale wote ambao hawataomba wasijewakidhani watahusika na masuala ya uhujumu uchumi, bali sheria itachukua mkondo wake. Aidha, alisisitika kesi zote mpya za uhujumu uchumi hawatahusika na msamaha huu, hii ikiwa ni onyo kwa wanaotaka kuhujumu nchi kuacha.

Watanzania tuwapokee kwa mikono mawili watanzania wenzetu waliokiri na kurejesha fedha  kwa roho safi. Tushirikiane nao katika hali na mali na kuhakikisha tunaijenga nchi yetu, nina hakika nchi ya maziwa na asali tutaifikia hivi punde kwa kuwa dalili za mvua ni mawingu. 

Tukumbuke  yaliyotokea serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Uongozi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo baadhi ya watanzania walikula njama za kuingia madarakani isivyo halali mwaka 1971. Wahusika takribani nane walikamatwa na kuwekwa ndani na kuhukumiwa kifungo cha maisha japo adhabu yake ilikuwa kunyongwa na miezi kadhaa baadaye alitoa msamaha na kuwaachia huru bila masharti yeyote.

Hii ilimletea sifa ya pekee duniani ni kiongozi aliyeongoza kwa kusamehe watu waliotaka kumuondoa madarakani  isivyo halali . Fatilia historia ya wahaini popote duniani hakuna aliyewaachia huru bali Babawa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Ambapo pia aliamua kuondoka madarakani kwa hiari yake mwenyewe mwaka 1985 na kumuachia kijiti cha uongozi Rais wa Awamu ya Pili Mhe. Ali Hassan Mwinyi, kitu ambacho kwa serikali za Afrika ilikuwa ni ndoto ya mchana kamwe hakikuwahi kutokea. Huyu ndiye Baba wa Taifa la Tanzania Pumzika kwa Amani Mwalimu.
04 Oktoba 2019

author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana