Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii.
WATU 18 wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni wakikabiliwa na shitaka moja la kufanya kazi za ununuzi na ugavi bila ya kusajiliwa na Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB).
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa na Mwanasheria wa Bodi ya wataalumu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), Suleiman Mnzava amewataja washtakiwa hao kuwa ni Jema Mbugi, Julieth Daniel, Jeremiah Mafuru, Lucy Wanne, Odillo Benedict, Bibiana Romanus, Bahati Wonnandi, Raphael Waryana, Joseph Mhere na Victor Kilonzo, Moshi Mohamed, Avitus Rutayuga, Esther Reyemamu, Ruth Mwaipyana, Beatrice Mushi, Julieth Mwihambi, Geogre Lyimo na Estonia Kalokola.
Mbele ya Hakimu Mkazi, Hudi Hudi imedaiwa kuwa kati ya Februari 11 na 15, 2019, katika ofisi mbalimbali jijini Dar es Salaam washtakiwa hao walikutwa wakifanya kazi za ununuzi na ugavi bila ya kusajiliwa na Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi(PSPTB) huku wakijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.
Aidha, upande wa mashtaka umeiomba mahakama itoe hati ya kukamatwa kwa washtakiwa Mehere, Mohamed, Mwaipyana na Mwihambi ambao hawakuwepo mahakamani hapo leo. Hata hivyo, washtakiwa wamekana kutenda kosa hilo na upande wa mashtaka umedai kuwa hauna pingamizi la dhamana dhidi ya washtakiwa.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo ameiomba mahakama ipange tarehe nyingine ili washtakiwa hao waweze kusomewe maelezo ya awali.
Washtakiwa hao wako nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ambapo mahakama iliwataka kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua kutoka Ofisi ya Serikali ya Mtaa na awe na kitambulisho cha Taifa. Pia ametakiwa kusaini bondi ya Shilingi Milioni 5 kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 21, 2019 kwa ajili ya kutajwa.
Baadhi ya wafanyakazi waliokuwa wanafanyakazi za ununuzi na ugavi bila kusajiliwa na Bodi ya wataalumu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) wakitoka kwenye chumba cha mahakama ya Kinondoni mara baada ya kufikishwa na Bodi hiyo.
Mwanasheria wa Bodi ya wataalumu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), Suleiman Mnzava akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwapandisha kizimbani wafanyakazi waliokuwa wanafanyakazi za ununuzi na ugavi bila kusajiliwa na bodi hiyo leo katika mahakama ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Post a Comment