Mtaalamu wa zamani wa masuala ya Russia katika Ikulu ya Marekani White House amesema, bughudha zinazomwandama kutokana na kukubali kutoa ushahidi katika kamati ya Kongresi kuhusu kashfa ya Ukrainegate zimefikia kileleni kwa kufika hadi ya kutishiwa kuuawa.
Fiona Hill, ambaye alikuwa mkurugenzi mwandamizi wa masuala ya Ulaya na Russia katika Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani (NSC) amesema, amekuwa akiandamwa na kampeni za bughudha na vitisho ikiwemo kutishiwa kuuawa, zilizofikia kileleni baada ya kukubali kutoa ushahidi mbele ya kamati ya bunge la Marekani inayofuatilia kumsaili na kumuuzulu rais wa nchi hiyo Donald Trump.
Katika ushahidi aliotoa mbele ya Kongresi, ambao matini yake kamili ilitolewa hadharani siku ya Ijumaa, afisa huyo mwandamizi wa zamani wa White House ameongeza kuwa, anga ya woga na hofu inatawala miongoni mwa wafanyakazi wa serikali ya Marekani kwa walio tayari kutoa ushirikiano kwa kamati inayochunguza kashfa ya Ukraingate.
Wakati huohuo, Luteni Kanali Alexander Vindman, ambaye ni mkurugenzi wa sasa wa Ikulu ya White House anayehusika na masuala ya Ulaya katika Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani amekiri kuwa, Trump alimrubuni kivitisho Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine katika mazungumzo ya simu waliyofanya mwezi Julai kwa ajili ya kujinufaisha binafsi kisiasa.
Imeripotiwa kuwa katika mazungumzo ya simu aliyofanya Trump mwezi Julai mwaka huu na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine, rais huyo wa Marekani alimtaka kiongozi huyo ampatie taarifa zitakazochafua haiba ya Joe Biden, anayewania kuteuliwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Democrat katika uchaguzi wa rais wa 2020.
Inasemekana kuwa Trump aliishurutisha Ukraine kufanya uchunguzi kuhusu ufisadi anaodaiwa kufanya Biden na mwanawe wa kiume Hunter Biden ili kukubali kuipatia nchi hiyo msaada wa dola milioni 250 kwa ajili ya masuala ya kijeshi.../
Post a Comment