Vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vimefanikiwa kuwaangamiza wapiganaji 25 wa kundi la wanamgambo wa ADF mashariki mwa nchi.
Mkuu wa operesheni hiyo, Jacques Ndurua ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, wanajeshi saba wa Kongo DR wameuawa pia katika makabiliano hayo na kundi hilo la kigaidi katika mji wa mashariki wa Beni, ulioko katika mkoa wa Kivu Kaskazini.
Amesema jeshi la nchi hiyo limefanikiwa pia kudhibiti maeneo manne ambayo yalikuwa ngome za wapiganaji hao mkoani Kivu Kaskazini, katika operesheni hiyo iliyoanza tangu Oktoba 30.
Katika miezi ya hivi karibuni, wanamgambo hao wa ADF ambao asili yao ni Uganda wamekuwa wakiwashambulia maafisa wa afya wanaopambana na ugonjwa hatari wa Ebola, mashariki mwa nchi.
Mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu, jeshi la DRC lilitangaza habari ya kuua wanamgambo wengine 26 wa ADF karibu na mji huo wa Beni ulioathiriwa na ugonjwa hatari wa Ebola, mashariki mwa nchi.
Juhudi za kupambana na ugonjwa wa Ebola mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimeendelea kukabiliwa na vizingiti kutokana na makundi hayo ya wanamgambo kushambulia madaktari na vituo vya afya vinavyotoa matibabu kwa wagonjwa wa maradhi hayo.
Post a Comment