Harakati hiyo iliyokuwa mwavuli wa vuguvugu la maandamano nchini Sudan yaliyopelekea kung'olewa madarakani Rais aliyehudumu kwa muda mrefu nchini humo Omar Hassan al Bashir imesema kuwa haipingi kukabidhiwa al Bashir kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ili ahukumiwe kwa jinai anazodaiwa kuhusika nazo jimboni Darfur.
Al Bashir ambaye alipinduliwa na jeshi mwezi Aprili mwaka huu kufuatia maandamano ya miezi kadhaa dhidi ya utawala wake kwa muda mrefu anasakwa na mahakama ya ICC yenye makao yake mjini Hague Uholanzi kwa tuhuma za mauaji ya kimbari, jinai za kivita na dhidi ya binadamu huko Darfur magharibi mwa Sudan.
Ibrahim Al Sheikh Kiongozi mwavuli wa harakati ya maandamano ya Vikosi vya Uhuru na Mabadiliko amesema kuwa wanachama wao wote wameafiki suala hilo. Omar al Bashir anashikiliwa katika jela moja huko Khartoum akikabiliwa na tuhuma za ufisadi. Alitawala Sudan kwa miongo mitatu baada ya kutwa madaraka katika mapinduzi yaliyojiri nchin humo mwaka 1989. Makundi ya kimataifa ya haki za binadamu, makundi ya waasi yaliyopigana dhidi ya vikosi vya al Bashir kwa miaka kadhaa na wanaharakati mbalimbali wamekuwa wakisisitiza juu ya ulazima wa kufikishwa Omar Hassan al Bashir katika mahakama ya ICC. Baada ya kupinduliwa Aprili 11 mwaka huu; waendesha mashtaka wa mahakama ya mjini Hague kwa mara nyingine tena walitaka kupandishwa kizimbani al Bashir kutokana na mauaji ya umati yaliyotekelezwa jimboni Darfur.
Post a Comment