Washiriki katika marasimu ya maadhimisho ya tarehe 13 Aban kote nchini Iran wamesisitiza katika azimio lililotolewa mwishoni mwa maandamano hayo kuwa: Stratejia ya muqawama ulio hai mkabala na njama za Marekani na waitifaki wake ni jukumu la kidini na lengo lisilobadilika la Mapinduzi ya Kiislamu.
Azimio hilo lililotolewa mwishoni mwa marasimu ya maadhimisho ya tarehe 13 Aban ambayo ni Siku ya Taifa ya Kupambana na Uistikbari wa Dunia hapa Iran limeeleza kuwa: Wananchi wa Iran wanaitambua Marekani inayoporomoka na kusambaratika kuwa adui namba moja wa ubinadamu; na hawana pia imani na baadhi ya viongozi wa nchi za Ulaya.
Washiriki wa maadhimisho ya leo ya Aban 13 kote hapa Iran wametangaza pia uungaji mkono wao wa pande zote kwa mapambano ya mujahidina wa Palestina, wanamapambano wa Ansarullah wa Yemen mbele ya utawala wa Aal Saud, wananchi wanaokandamizwa wa Bahrain na Nigeria na Hizbullah na vilevile kwa mapambano yanayoendeshwa katika eneo.
Katika azimio hilo, wananchi wa Iran wamelaani pia njama za Marekani, utawala wa Kizayuni na utawala wa Aal Saud za kutumia vibaya matakwa ya wananchi, kuibua ghasia na machafuko huko Lebanon na Iraq, na kuchochea migawanyiko katika nchi za Kiislamu na mhimili wa muqawama.
Washiriki hao wamesisitiza pia ulazima wa kuwa macho nchi za eneo khususan Lebanon na Iraq mbele ya njama za maadui. Maadhimisho ya Siku ya Taifa ya Kupambana na Ubeberu wa Kimataifa yamefanyika leo asubuhi katika miji elfu moja ya Iran ya Kiislamu kwa kuhudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi, wanachuo na viongozi wa serikali.
Post a Comment