Featured

    Featured Posts

MWONGOZO WA UWEKEZAJI WA MKOA WA MTWARA WAZINDULIWA


NA K-VIS BLOG/Khalfan Said, Mtwara
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amezindua Mwongozo wa Uwekezaji Mkoani Mtwara (MIG) katika Kongamano la Uwekezaji na Maonyesho ya Biashara lililofanyika kwenye viwanja vya Chuo Cha Ualimu Mtwara.
Mwongozo huo umetayarishwa na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) kwa kushirikiana na Mkoa chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
“Kuja kwenu Mtwara leo hii hamjapoteza nauli na muda wenu, mmekuja Mtwara mahali sahihi kwa uwekezaji na mtatumia nafasi ya leo kusikia nini kimeandaliwa kwa ajili ya kuwaambia fursa zipi zinapatikana mkoani Mtwara.” Amesema Waziri Mkuu Majaliwa
Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya Tano imedhamiria kwa dhati kuiondoa Tanzania kwenye uchumi wa chini kwenda Uchumi wa Kati na hakuna njia nyingine isipokuwa ni kuvutia uwekezaji, Serikali inakaribisha wawekezaji kuwekeza hapa nchini iwe ni Mtanzania au mgeni kutoka nje ya nchi atapokelewa ili aweze kuwekeza hapa nchini.
“Wakati nikizungumza na wakuu wa mikoa Juni 18, 2018 jijini Dodoma nilitoa maelekezo na dira ya kila mkoa kupata wawekezaji, niliagiza kila mkoa lazima ujipange kuhakikisha unatangaza fursa zilizopo katika mkoa.”Alifafanua Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Majaliwa alisisitiza Mikoa ambayo bado haijaandaa miongozo ya uwekezaji ifanye hivyo mara moja kabla mwaka huu haujaisha. Pia aliwaonya watumishi wanaokuwa vikwazo kwa wawekezaji waache mara moja na wanaobainika wachukuliwe hatua stahiki.
“Niipongeze Taasisi ya ESRF chini ya Mkurugenzi wake Dkt. Tausi Kida imefanya kazi kubwa na nzuri, baada ya kufanya utafiti imetoa tathmini ya nini kifanyike, wapi tufanye nini ili tuweze kufanikisha uwekezaji hapa nchini” Amesema Waziri Mkuu Majaliwa na kuongeza….Kila ninapokwenda kuzindua Miongozo ya Uwekezaji nimekuwa nikukutana na ESRF ikiongozwa na Dkt. Tausi Kida, hongera sana kwa kazi nzuri mnayofanya.” Alipongeza Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu pia ameipongeza UNDP kwa kufanya kazi kwa pamoja na Serikali na kuahidi kuwa Serikali itaunga mkono shughuli za UNDP ambazo Serikali ya awamu ya Tano na zile zilizotangulia daima zimekuwa zikifanya kazi kwa pamoja na UNDP na zinatambua mchango mkubwa unaotolewa na Taasisi hii ya kimataifa.
Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angela Kairuki. Wakati akimkaribisha Waziri Mkuu kuhutubia, Mhe. Kairuki alieleza hatua ambazo Serikali imechukua kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini na kupelekea Tanzania kupanda kutoka nafasi ya 144 hadi 141 kwenye urahisi wa kufanya biashara duniani.
Mawaziri wengine waliohudguria na kutoa neno ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa, na Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga.
Wakati akitoa salaamu, Mwenyeji wa Mkoa huo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa aliwakaribisha wageni waalikwa na kuelezea jinsi Mkoa ulivyojipanga kuwapokea na kuwasaidia wawekezaji. Pia alitoa fursa kwa Wakuu wa Mikoa jirani walihudhuria halfla hiyo ya uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa wa Mtwara kutoa neno. Waliohudhuria ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Chrintina Mdema na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi  Evarist Ndikilo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwakilishi Mkazi wa UNDP hapa nchini, Bi.Christine Musisi alisema UNDP itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi. Alisema UNDP itaendelea kusaidiana na Mikoa katika utekelezaji wa miongozo hii kwa kutoa ushauri wa kitaalam na rasilimali fedha panapohitajika.
Awali akiwasilisha Muhtasari wa Fursa za Uwekezaji katika Mkoa wa Mtwara katika Kongamano la Uwekezaji, Mtafiti Mkuu Mshiriki kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF) Dkt. Oswald Mashindano alisema ESRF ilifanya utafiti kwenye halmashauri zote za Mkoa wa Mtwara na utafiti huo ulibaini uwepo wa fursa nyingi za uwekezaji. Dkt. Mashindano alitaja timu ya wataalam kutoka ESRF walioshiriki kuandaa Mwongozo wa Uwekezaji ikijumuisha Prof. Haidari Amani, Bi. Margareth Nzuki, Bw. Mussa Mayala Martine, na Bw. James Kasindi.
Dkt. Mashindano alitaja fursa mbalimbali za uwekezaji ambazo zimepewa kipaumbele na mkoa. Fursa hizi ziko katika makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwekezaaji katika kilimo hasa korosho, kilimo cha umwagiliaji wa mpunga na miwa, ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji wa mpunga na mazao ya bustani; uwekezaji katika mifugo hasa ranchi na unenepeshaji wa mifugo; uwekezaji katika uvuvi hasa uvuvi ndani ya bahari kwa kutumia nyenzo na teknolojia za kisasa pamoja na ufugaji wa samaki; uwekezaji katika viwanda hasa Kuchakata Korosho na mazao mengine kama mhogo, nazi, choroko, mbogamboga na matnda, kuchakata na kufungasha chimvi, Chakula cha Mifugo, Kuchakata Samaki, Kiwanda cha Kutengeneza Maji ya Chupa nk.
Fursa za uwekezaji katika eneo la miundombinu zilijumuisha ujenzi wa jengo kwa ajili ya matengenezo na maegesho ya ndege, stendi za kisasa, ujenzi wa kituo cha michezo ikijumuisha uwanja wa mpira, masoko ya kisasa nk. Aidha Dkt. Mashindano alitaja makundi mengine ya fursa za uwekezaji kuwa ni pamoja na uwekezaji katika utalii akilenga uwekezaji kwenye fukwe, michezo ya baharini, ujenzi wa hoteli, majumba ya starehe, kambi za watalii, kuendeleza maeneo ya kihistoria nk. Pia zilibainishwa fursa za uwekezaji katika huduma za kijamii zikijumuisha afya na elimu. Kwa upande wa afya kuna fursa ya ujenzi wa hospitali na kiwanda cha kutengeneza maji ya wagonjwa na vifaa tiba. Kwa upande wa elimu alitaha fursa ya kuendesha chuo maalum cha ujuzi pamoja na shule binafsi za kisasa.
Baada ya uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji washiriki walipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya uwekezaji Mkoani Mtwara.
Maonesho ya biashara na Uwekezaji yanafikia kilele leo Novemba 3, 2019.
 Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa (watatu kushoto), akikata utepe, kuzindua Mwongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Mtwara (MIG), kwenye Chuo Cha Ualimu Mtwara Novemba 1, 2019. Wanaoshuhudia ni kutoka kulia ni Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga, Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dkt. Tausi Kida, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angela Kairuki  Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Bi. Christine Msisi na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe.Gelasius Byakanwa. 
 Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa (katikati), akionyesha nakala za Mwongozo wa Uwekezaji Mkoani Mtwara (MIG), baada ya kuuzindua kwenye Chuo Cha Ualimu Mtwara Novemba 1, 2019. Wanaoshuhudia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angela Kairuki (wapili kulia), Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Bi. Christine Msisi (wapili kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe.Gelasius Byakanwa (wakwanza kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dkt. Tausi Kida. 
 Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida, huku Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angela Kairuki (katikati) akishuhudia, mara baada ya Waziri Mkuu kuzindua Mwongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Mtwara Novemba 1, 2019.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida, huku Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angela Kairuki (katikati) akishuhudia, mara baada ya Waziri Mkuu kuzindua Mwongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Mtwara Novemba 1, 2019.
 Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akihutubia kongamano hilo na kisha kuzindua Mwongozo huo Novemba 1, 2019.
Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchi Bi. Christine Msisi akitoa hotuba yake.
 Viongozi waandamizi wa ESRF walioshiriki katika utafiti huo kutoka kushoto,Bw. Mussa Mayala Martine,  Dkt. Oswald Mashindano na Bi. Margareth Nzuki.
 Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akimpatia nakala ya Mwongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Mtwara (MIG), Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga huku Mhe. Kairuki (katikati) akishuhudia. 
 Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akimpatia nakala ya Mwongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Mtwara (MIG), Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa huku Mhe. Kairuki (katikati) akishuhudia. 
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akimpatia nakala ya Mwongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Mtwara (MIG) Mwakilishi Mkazi wa UNDP hapa nchini, Bi. Christine Msisi. Wanaoshuhudia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Mhe. Angela Kairuki (wapili kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida. Mwongozo huo umetayarishwa na (ESRF) kwa kushirikiana na Mkoa wa Mtwara chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana