Harakati ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah imetangza kuwa imeshambulia taasisi za shirika kubwa zaidi la mafuta la Saudi Arabia la Aramco katika eneo la Jizan karibu na Bahari Nyekundu.
Msemaji wa jeshi la Yemen, Yahya Sarie amesema kuwa mashambulizi hayo yamefanyika kujibu hujuma na mashambulizi ya anga yanayoendelea kufanywa na ndege za kivita za Saudia dhidi ya taifa la Yemen.
Sarie amesema kuwa, jeshi la Yemen limefanya mashamblizi ya aina yake kwa kutumia makombora dhidi ya taasisi za Aramco huko Jizan, viwanja vya ndege vya Abha na Jazan na kambi ya jeshi ya Khamis Mushait na maeneo mengine muhimu ndani ya ardhi ya Saudi Arabia.
Msemaji wa jeshi la Yemen ameongeza kuwa, jeshi hilo limeendelea kusonga mbele katika mkoa wa Marib na kufanikiwa kukomboa wilaya za mkoa huo na ule wa al Jouf na maeneo mengine yenye ukubwa wa kilomita 2500 kutoka kwa vibaraka wa Saudia na waitifaki wake. Amesema kuwa jeshi la Yemen limefanikiwa kuangamiza brigedi tano za wapiganaji wa adui katika wilaya ya Sirwah na katika mkoa wa al Jouf katika operesheni ya kijeshi iliyopewa jina la al Bunyanul Marsus".
Yahya Sarie amesisitiza kuwa jeshi la Yemen litaendeleza mapambano hadi litakapofanikiwa kukomboa ardhi yote ya nchi hiyo na kuwafukuza kikamilifu wavamizi wa kigeni.
Maelfu ya raia wa Yemen wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi tangu Saudi Arabia na washirika wake walipoanzisha mashambulizi dhidi ya taifa la Yemen mwezi Machi mwaka 2015.
Post a Comment