Ripoti mpya zinaelezea rekodi mpya ya mashambulizi ya Marekani nchini Afghanistan.
Jumamosi iliyopita vyombo vya intelejensia vya serikali ya Afghanistan vilitangaza kuwa, mwaka 2019 askari wa Kimarekani walitekeleza mashambulizi 7,423 katika maeneo tofauti ya kiraia ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo mashambulizi ya mwaka jana ndio yalivunja rekodi katika miaka 10 iliyopita. Aidha duru za kikosi cha anga cha jeshi la Marekani zinaonyesha kwamba katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, mashambulizi ya jeshi hilo vamizi hayakufikia kiwango sawa na hicho, katika hali ambayo askari hao wa Kimarekani wamekuwa wakishambulia mara kwa mara maeneo ya raia wa kawaida.
Hivi karibuni pia Umoja wa Mataiafa ulionyesha wasi wasi wake kutokana na mauaji ya raia wa kawaida yanayosababishwa na mashambulizi ya jeshi la Marekani nchini Afghanistan. Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, mashambulizi ya anga ya jeshi la Marekani nchini Afghanistan mwaka 2018 yalisababisha mauaji ya raia 393 na wengine 239 kujeruhiwa. Marekani na washirika wake waliivamia kijeshi Afghanistan kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi hapo mwaka 2001, hata hivyo uvamizi huo umepelekea kuongezeka machafuko, ugaidi na uzalishaji wa madawa ya kulevya. Viongozi na wananchi wa Afghanistan mara nyingi wametaka askari hao wa kigeni wanaoongozwa na Marekani waondoke katika ardhi ya taifa hilo la Asia lakini bila mafanikio yoyote.
Post a Comment