Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ujumbe maalumu wa mkono wa pole kufuatia kufariki dunia wananchi kadhaa wakati wa kusindikiza jeneza la mwili mtoharifu wa shahidi Kamanda Qassem Soleimani wakati wa maziko yake yaliyofanyika mkoani Kerman na vile vile wananchi walioaga dunia katika tukio la ajali ya ndege ya abiria iliyoanguka hapa mjini Tehran.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameeleza katika ujumbe huo: "Tukio chungu na la kuhuzunisha la kupoteza maisha idadi kadhaa wa Wairani wakati wa kumsindikiza shahidi mwenye hadhi kubwa Luteni Jenerali Qassem Soleimani, na vile vile tukio la msiba la kuanguka ndege ya abiria na kufariki dunia abiria Wairani na wasio Wairani ni matukio mawili ya kuhuzunisha yaliyojiri katika siku hizi mbili."
Katika ujumbe wake huo, Ayatullah Khamenei amezifariji familia zilizofikwa na misiba hiyo; na sambamba na kubainisha huzuni na masikitiko makubwa aliyonayo, amemwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awape subira na uvumilivu wafiwa na rehma na maghufira wote waliofariki dunia.
Kufuatia matukio mawili hayo ya misiba, serikali ya Iran imetoa taarifa na kuitangaza leo Alkhamisi kuwa ni siku ya maombolezo.
Watu kadhaa walifariki dunia na wengine wengi walijeruhiwa siku ya Jumanne kutokana na mbinyo na msongamano mkubwa uliotokea katika shughuli ya maziko ya shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu yaliyofanyika mkoani Kerman kusini mwa Iran.
Jana asubuhi pia ndege moja ya abiria ya shirika la ndege la Ukraine ilianguka karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Imam Khomeini hapa mjini Tehran, ambapo abiria wote 167 na wahudumu 9 waliokuwemo ndani yake walifariki dunia.
Wengi wa abiria hao walikuwa raia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mbali na abiria wengine wa mataifa mengine kadhaa.
Ubalozi wa Ukraine mjini Tehran umetangaza kuwa, hitilafu za mitambo ndicho chanzo cha kuanguka ndege hiyo kando kando ya mji wa Tehran.../
Post a Comment