Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Guinea- Bissau jana imemthibitisha Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo Umaro Cissoko Embalo kuwa mshindi wa uchaguzi wa Rais baada ya Mahakama Kuu nchini humo wiki iliyopita kutilia shaka matokeo yaliyokuwa yametangazwa.
Ijumaa iliyopita Mahakama Kuu ya Guinea- Bissau ilitaka kutolewa maelezo kuhusu matokeo ya uchaguzi wa rais baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini humo kutangaza matokeo ya mwisho yaliyoonyesha Embalo ameibuka na ushindi wa asilimia 54 ya kura akimpita mpinzani wake Domingos Simoes Pereira aliyepata asilimia 46 ya kura.
Tume hiyo ya uchaguzi imeongeza kuwa kilichobaki sasa ni kukamilisha taratibu za kumuapisha Rais mpya. Umaro Cissoko Embalo Waziri Mkuu wa zamani na Jenerali wa zamani wa jeshi nchini Guinea- Bissau amepongezwa kufuatia ushindi huo wa uchaguzi huku mpinzani wake na mgombea wa chama tawala Pereira akihoji matokeo hayo. Amesema matokeo yaliyotangazwa na kuonyesha kushinda hasimu wake Embalo yamegubikwa na udanganyifu.
Post a Comment