Nchi ya Libya imo katika siku ngumu na mgogoro mkubwa, na vita na mapigano makali yameendelea kushuhudiwa nchini humo licha juhudi kubwa za kimataifa zinazofanyika kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa mgogoro huo.
Kamanda wa wanamgambo wanaojiita jeshi la taifa la Libya, Jenerali Khalifa Haftar ambaye anadhibiti maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo ametangaza kuwa, hakubali usitishaji vita endelevu; kwa msingi huo wapiganaji wa kundi hilo wameanzisha tena mashambulizi dhidi ya mji wa Tripoli. Wakati huo huo Rais wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya, Fayez al Sarraj ametangaza kuwa, ataheshimu wito uliotolewa katika mkutano wa Berlin wa kusitisha vita na kufuatilia mazungumzo ya kisiasa lakini hatakaa tena kwenye meza ya mazungumzo na Jenerali Khalifa Haftar. Wakati huo huo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limezitaka pande zote zinazozozana nchini Libya kujiunga na makubaliano ya kusitisha vita.
Kwa sasa Libya imekuwa medani ya vita vya pande zote ndani ya nchi na katika medani ya kimataifa. Ndani ya nchi, wapiganaji wa Khalifa Haftar wameanzisha tena mashambulizi makali dhidi ya maeneo ya kusini mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli. Vilevile wamesimamisha shughuli zote za taasisi za mafuta na uuzaji nje bidhaa hiyo kupitia bandari za Libya. Katika uwanja huo Shirika la Mafuta la Libya limetangaza kuwa, kufungwa kwa bandari za mafuta za Libya kumepunguza uuzaji nje wa mapipa laki nane ya mafuta kwa siku, suala ambalo lina maana ya kupungua pato lenye thamani ya dola milioni 55 kila siku.

Haftar ambaye anasaidiwa kijeshi la nchi kama Saudi Arabia, Imarati na Misri amekataa kusaini makubaliano ya kusitisha vita yaliyotayarishwa katika kikao cha amani cha tarehe 13 mwezi huu mjini Moscow na hakushiriki katika mkutano wa tarehe 19 Januari wa Berlin uliokuwa na lengo la kutafuta suluhisho la mgogoro wa Libya.
Ahmad Khalifa ambaye ni ripota wa televisheni ya al Jazeera ya Qatar anasema: "Vita na mashambulizi dhidi ya mji wa Tripoli yameingia mwezi wa 9 sasa na kamanda wa linalojiita jeshi la taifa la Libya, Khalifa Haftar ambaye wapinzani wake wanafanya jitihada za kumfutilia mbali kisiasa na kumuarifisha kama mtenda jinai za kivita, anaendelea kushikilia misimamo yake ya kikaidi na hayuko tayari kukubali utatuzi wa amani wa mgogoro huo."
Katika upande mwingine Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa inayopambana na wapiganaji wa Haftar na kulinda mji wa Tripoli, imeomba msaada wa kijeshi wa Uturuki ambayo imekubali kutuma vikosi vyake nchini Libya. Suala hili limekosolewa sana na Haftar na nchi zinazomuunga mkono.

Sambamba na mapigano hayo ya ndani, kinyang'anyiro kingine juu ya Libya kinashuhudiwa katika medani ya kimataifa ambako hakushuhudiwi mtazamo mmoja kwa ajili ya kutatua mgogoro wa nchi hiyo na kila moja kati ya nchi zinazojihusisha na mgogoro wa ndani wa Libya inaunga mkono moja kati ya pande mbili zinazozozana. Vilevile mkutano wa Berlin na hatua ya Jenerali Haftar baada ya mkutano huo vinaonesha kwamba, kinachofuatiliwa na pande mbili hasimu na wafadhili wao si njia halisi ya utatuzi wa mgogoro huo bali ni kudhamini maslahi yao katika meza yenye tonge nono la mafuta na gesi ya Libya.
Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, kufuatia ongezeko la harakati za wachezaji wapya kama Ujerumani, Russia na Uturuki katika kuwania utajiri wa maliasili ya Libya sambamba na harakati za wachezaji wa zamani katika mgogoro wa nchi hiyo kama Saudi Arabia, Imarati, Misri na Ufaransa, kwa sasa kunashuhudiwa mpambano mpya baina ya pande mbili hasimu na wafadhili wao. Katika mazingira kama haya ni vigumu sana kudhani kwamba mgogoro huo utapatiwa ufumbuzi katika siku za hivi karibuni.

Shadan Hammam ambaye ni mtaalamu wa masuala ya nchi za Kiarabu anasema: "Mkutano wa Berlin haukuweza kutia ufa katika ukuta wa mgogoro wa Libya, na hitilafu za kimataifa kuhusu mgogoro huo zingali zinazuia usitishaji vita halisi nchini humo."
Post a Comment