Waziri Heiko Maas amesema ni katika maslahi ya kila mmoja kuendeleza mapambano dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS, kama sehemu ya muungano wa kimataifa nchini Iraq, ili kulinda mafanikio yaliofikiwa huko awali.
"Ni muhimu kwamba sisi kama washirika wa muungano dhidi ya IS tunaendelea kuwepo nchini Iraq na ni muhimu pia kwa Iraq na tunafanya mazungumzo na serikali kuhusu umuhimu wa kubakia kwa vikosi vya kimataifa licha ya uamuzi wa bunge kutaka vikosi hivyo viondoke," alisema Maas na kuongeza kuwa "tunahofia kwamba iwapo vikosi vya kimataifa vitaondoka kitisho cha IS kitarejea kuwa kikubwa."
Heiko Maas alitoa matamshi hayo katika mkutano wa waandishi habari aliouhutubia pamoja na mwenzake wa Jordan Ayman Al Safadi katika mji mkuu wa Amman.
Ujerumani iliwahamisha wanajeshi wake 35 wanaohudumu nchini Iraq katika mataifa jirani ya Jordan na Kuwait siku ya Jumanne, kufuatia tafrani iliyosababishwa na kitendo cha Marekani kumuuwa Jenerali wa Iran katika shambulio la ndege mjini Baghdad wiki iliyopita.
Waziri Maas akikutana na mwenzakewa Jordan Ayman Safadi mjini Amman, Jordan, 13.01.2020.
Aitaka Iran kuacha kuingilia mizozo ya wengine
Mauaji ya kamanda huyo wa kikosi maalumu cha jeshi la ulinzi wa mapinduzi cha Quds, Qassem Soleimani yamechochea pakubwa mzozo wa kikanda na kuzidisha uhasama kati ya Washington na Tehran. Ujerumani ina kikosi kidogo cha wanajeshi wapatao 120 nchini Iraq, ingawa wengi wao wako nje ya mji wa Baghdad.
Maas ametumia mkutano huo kuitaka Iran kuacha kujiingiza katika mizozo ya kanda hiyo, akisema iwapo nchi hiyo inataka kutuliza mzozo, inapaswa kuacha uchochezi ikiwemo pamoja na nchini Iraq.
Jordan ni mshirika muhimu wa mataifa ya Magharibi katika mapambano dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu na hivi sasa inahifadhi zaidi ya Wasyria milioni moja waliokimbia vita nchini mwao, wakiwemo watu 650,000 waliosajiliwa kama wakimbizi na shirika la UNHCR.
Maas alitarajiwa kuwatembelea wanajeshi wa Ujerumani walioko katika kambi ya jeshi la anga ya Al-Azraq, umbali wa kilomita 90 mashariki mwa mji wa Amman, kabla ya kurejea Ujerumani.
Kawaida ndege za uchunguzi za Ujerumani zinazoendesha opereseni zake nchini Syria na Iraq zinatokea uwanja wa Al-Azraq lakini kwa sasa zimesimamishwa baada ya bunge la Iraq kupitisha uamuzi wa kutaka kuondolewa kwa vikosi vya kimataifa vinavyopambana dhidi ya Dola la Kiislamu.
Vyanzo: Mashirika
Post a Comment