Charles James, Michuzi TV
DAKIKA 300 zimetosha kutumika na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) kumhoji aliyekua Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe Kangi Lugola juu ya tuhuma zinazomkabili.
Mbunge wa Jimbo la Mwibara mkoani Mara, Kangi aliwasili katika ofisi za TAKUKUR saa 1:24 asubuhi ya leo jijini Dodoma huku akiwa na ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM kama ilivyo kawaida yake.
Mwingine ambaye amefika kuhojiwa na TAKUKURU ni aliyekua Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu ambaye ameteuliwa kuwa Balozi hivi karibuni na Rais Dk John Magufuli.
Baada ya kumaliza kuhojiwa Lugola aliondoka na gari yake aina ya Land Cruiser VX huku akiwaeleza wandishi wa habari kuwa ni mzima wa afya.
" Mimi sijambo, ni mzima wa afya. Kwa leo siwezi kuongea chochote," hizo ni baadhi ya kauli za Lugola kwa wandishi wakati akitoka nje baada ya kumaliza mahojiano.
Lugola, Meja Jenerali Kingu na aliyekua Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto, Thobias Andengenye wanahojiwa na TAKUKURU kufuatia kashfa ya watendaji wa wizara hiyo kutia saini makubaliani ya zabuni ya kununua vifaa vya zimamoto vyenye thamani ya Euro Milioni 408 sawa na Shilingi Trilioni Moja bila kufuata utaratibu wa sheria.
Aliyekua Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akitoka nje ya ofisi za TAKUKURU baada ya kumaliza kuhojiwa juu ya tuhuma zinazomkabili.
Aliyekua Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akipanda kwenye gari yake tayari kwa kuondoka baada ya kumaliza kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa leo jijini Dodoma.
Aliyekua Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto, Thobias Andengenye akiwasilia kwenye Ofisi za Makao Makuu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mchana huu tayari kwa mahojiano juu ya tuhuma zinazomkabili.
Post a Comment