Msemaji wa ikulu ya Afghanistan ametangaza habari ya kutofikiwa mapatano katika mazungumzo kati ya kundi la Taliban na Marekani nchini Qatar.
Sadiq Sadiqi ameyasema hayo katika kikao na waandishi wa habari mjini Kabul na kuongeza kwamba, hakukufikiwa maendeleo yoyote yale katika mazungumzo kati ya mwakilishi wa Marekani na kundi la Taliban nchini Qatar kuhusiana na kupunguzwa mapigano na utumiaji mabavu pamoja na usitishaji vita. Msemaji wa Ikulu ya Afghanistan aidha amesisitizia udharura wa kukubaliwa usitishaji vita na kusema kuwa, ili kufikiwa usalama nchini Afghanistan ni lazima kundi la Taliban liingie katika mazungumzo ya moja kwa moja na serikali ya Kabul. Mwishoni mwa kikao hicho na waandishi wa habari, Sadiq Sadiqi alisema kuwa, kuhitimishwa vita na kurejea usalama nchini Afghanistan ni suala linalopewa kipaumbele na serikali ya Kabul. Mazungumzo kati ya wawakilishi wa kundi la Taliban na Marekani yamefanyika kwa duru 11 ambapo pande mbili hadi sasa hazijawa tayari kuishirikisha serikali ya Afghanistan kwenye mazungumzo hayo. Aidha kuvunjika duru mpya ya mazungumzo kati ya Washington na Taliban nchini Qatar, kumejiri ambapo ripoti mpya zilizoenezwa zinaonyesha kwamba pande mbili zilifikia mwafaka kuhusu muswada wa azimio la amani, na kwamba muswada huo upo tayari kwa ajili ya kutiwa saini.
Hata hivyo kwa kuzingatia kuwa, jibu hasi la kundi la Taliban kuhusu takwa la hivi karibuni la White House katika kulitaka kundi hilo lipunguze vitendo vya utumiaji mabavu nchini Afghanistan, ndio maana duru hiyo ya mazungumzo ikashindwa kufikia natija hiyo. Kabla ya hapo Zalmay Khalilzad, mwakilishi maalumu wa Marekani katika masuala ya Afghanistan alikuwa amelitaka kundi la Taliban kupunguza vitendo vya utumiaji mabavu na mapigano ambapo hata hivyo alipata jibu hasi kutoka kwa kundi hilo. Kiongozi wa kundi la Taliban alisisitiza kwamba, usitishaji mapigano nchini Afghanistan unaweza kufikiwa pale tu Marekani itakapotia saini makubaliano ya amani sambamba na kuondoa askari wake kutoka ardhi ya nchi hiyo. Suala la Taliban kukataa kupunguza mapigano linaonyesha kwamba kundi hilo halipo tayari kukubali kirahisi matakwa ya Marekani, na hivyo limeazimia kwa dhati kuendeleza vita hadi pale kutakapotiwa saini mapatano ya amani na kuondoka askari wa Marekani kutoka nchi hiyo. Kutokana na tabia ya kila mara ya Marekani ya kukiuka ahadi katika mapatano yake na nchi tofauti za dunia na pia kutotekeleza kwake ahadi, ndio maana Taliban haipo tayari kupunguza mapigano na kisha kuhitimisha vita kabla ya kutiwa saini makubaliano ya amani na Marekani na kisha kuondoa askari wake nchini humo.
Hata hivyo upinzani dhidi ya pendekezo la Marekani la kutaka kupunguzwa mapigano nchini Afghanistan, halikomei tu kwa kundi la Taliban, bali hata serikali ya Kabul pia imepinga pendekezo hilo. Serikali ya Afghanistan imetangaza kwamba kupunguzwa tu mapigano ni jambo lisilo na maana, bali kile serikali inachokitaka ni kuhitimishwa kabisa vita. Kwa mtazamo wa viongozi wa serikali ya Kabul, pendekezo la Marekani la kulitaka kundi la Taliban kupunguza mashambulizi, ni ishara ya kupuuza mahitaji ya nchi hiyo ya kuainisha stratijia na matakwa yake ya kitaifa kwa ajili ya kuimarisha usalama na amani. Serikali ya Afghanistan inaamini kwamba kinyume na madai yake, Marekani haina nia ya kweli ya kusaidia juhudi za kurejesha usalama na utulivu nchini humo na kitendo cha kuiondoa Kabula katika mazungumzo ya amani na kundi la Taliban, kimsingi kinakwenda kinyume kikamilifu na maslahi na haki ya kujitawala wananchi wa Afghanistan. Serikali ya Kabul kwa mara kadhaa imetangaza kwamba mapatano yoyote ya amani kati ya Marekani na Taliban yatakayofikiwa bila kuishirikisha serikali, hayatokuwa halali kama amabavyo pia hata utekelezwaji wake hautoyumkinika.
Post a Comment