Wazir wa Habari na Teknolojia ya Mawasiliano ICT wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa majaribio ya awali yamefanyiwa kwa mafanikio Satelaiti mbili za Zafar (Ushindi) na kwamba zitatumwa katika anga za mbali hivi karibuni.
Akizungumzia suala hilo kupitia ujumbe aliouandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Azari Jahromi amesema kwamba Zafar nambari 1 na 2 zilipelekwa jana katika kituo cha anga za mbali katikati mwa Iran kwa ajili ya maandalizi ya kutumwa angani.
Amesema satelaiti hizo ambazo zimeundwa na wanasayansi vijana wa Iran tayari zimefanyiwa majaribio kwa mafanikio na kwamba hatua za kuzituma katika anga za mbali zitaanza hivi karibuni.
Satelaiti ya Zafar ambayo imetengenezwa na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Iran ina uzito wa kilogramu 113 na ina mitambo ya kudhibitiwa na kuendeshwa kutokea mbali ikiwa ni pamoja na kamera ambazo zina uwezo wa kutuma data na maelezo yanayohusiana na maliasili na masuala ya mazingira. Tofauti iliyopo kati ya Zafar 1 na 2 ni kuwa ya pili ina kamera zanazotuma data na picha za rangi.
Mwezi Septemba mwaka uliopita, Wizara ya Fedha ya Marekani iliiwekea vikwazo sekta ya anga za mbali lakini licha ya hayo Iran imepiga hatua na kupata mafanikio makubwa katika uwanja huo.
Iran ilirusha angani satelaiti yake ya kwanza iliyotengenezwa humu nchini kwa jina la Omid mwaka 2009. Pia ilituma katika anga za mbali kapsuli iliyobeba kiumbe hai mwaka 2010 ikitumia roketi ya Kavoshgar (Explorer) 3.
Post a Comment