Mbunge wa Muungano wa Al Fath katika Bunge la Iraq amesema maandamano ya kesho Ijumaa nchini Iraq ni sawa na kura ya maoni ya wananchi wanaopinga kuwepo wanajeshi wa Marekani katika nchi hiyo.
Mohammad al Baldawi, amesema kuwa, maandamano yaliyopangwa kufanyika kesho Ijumaa kote Iraq yatabainisha wazi msimamo wa wananchi kuhusu uwepo wa wanajeshi wa Marekani katika ardhi ya Iraq. Ameongeza kuwa: "Jitihada za Marekani za kuendelea kubakia kijeshi Iraq zimefeli."
Kesho Ijumaa 24 Januari wananchi wa Iraq wanatazamiwa kujitokeza kwa wingi katika miji mbali mbali ya nchi hiyo baada ya Sala ya Ijumaa kushiriki katika maandamano yaliyo dhidi ya Marekani. Viongozi wa kisiasa, kidini na kitaifa nchini Iraq wametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika maandamano hayo ya kihistoria.

Kufuatia hujuma ya kigaidi ya Marekani ya Januari 3 iliyopelekea kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Kamanda wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq (Al Hashd al Shaabi) na wenzao wanane, Bunge la Iraq mnamo Januari 5 lilipitisha kwa kauli moja muswada wa kutaka wanajeshi wa Marekani waondoke nchini humo.
Viongozi wengi wa Iraq akiwemo Waziri Mkuu Adel Abdul Mahdi, wameunga mkono uamuzi huo wa bunge na wanasisitiza kuwa wanajeshi wa Marekani wanapasa kuondoka Iraq mara moja.
Post a Comment