Hatua ya hivi karibuni ya troika ya Ulaya inayozijumuisha nchi za Ujerumani, Ufaransa na Uingereza ya kuanza kutekeleza utaratibu wa kutatua tofauti ndani ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA, ambayo imeanzishwa kwa mashinikizo ya Marekani, imekabiliwa na radiamali kali ya Iran.
Katika uwanja huo, Mohammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekosoa mwenendo wa troika ya Ulaya kuhusiana na mapatano hayo ulioathiriwa na siasa za Marekani. Katika ujumbe alioandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter likiwa ni jibu kwa matamshi ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump wa Marekani katika kikao cha mjini Davos, Uswisi, Zarif amesema: "Wakati wiki iliyopita nchi tatu za Ulaya zilipoyauza mapatano yaliyosalia ya nyuklia kwa lengo la kukwepa ushuru wa Trump, nilizionya kuwa hatua hiyo itaufanya uchu wake uwe mkali tu zaidi. Nchi za Ulaya baada ya kuuza hadhi yao na kupoteza itibari yao ya kimaadili na kisheria, sasa zimekabiliwa na kitisho cha ushuru mwingine. Lililo bora kwa Ulaya ni kushughulikia mamlaka yao ya kujitawala."
Alichoashiria Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ni misimamo legevu ya nchi za Ulaya ambazo licha ya ukosoaji mkubwa wa maneno zinaofanya kwa siasa na hatua za serikali ya Trump, kivitendo, hazina uthubutu wa kukabiliana na serikali ya Washington, na pale zinapokabiliwa na vitisho vya White House, huishia kurudi nyuma na kulegeza msimamo.

Mfano wa wazi wa suala hilo ni hatua iliyochukuliwa tarehe 14 Januari na nchi tatu za Ulaya ya kuanzisha mchakato wa kutatua tofauti ndani ya JCPOA ambapo baadaye ilifichuka na kubainika kuwa nchi hizo zilichukua uamuzi huo kutokana na vitisho vya Trump vya kuyapandishia ushuru magari yanayoingizwa Marekani kutoka Ulaya. Mbali na uafriti na ukwamishaji mkubwa inaofanya, Marekani imefanya kila iwezalo kuyasambaratisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Hii ni kusema kuwa baada ya hatua hiyo ya nchi za Ulaya ilibainika kuwa mashinikizo makali ya Washington ndio yaliyozifanya nchi hizo zichukue hatua hiyo. Katika uwanja huo tarehe 17 ya mwezi huu Brian Hook, mwakilishi maalumu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani katika masuala ya Iran, alikiri kwamba mashinikizo ya Marekani kwa nchi za Ulaya ndio yaliyozipelekea nchi hizo kuanzisha mfumo wa utatuzi wa tofauti ndani ya JCPOA.
Umoja wa Ulaya na troika ya umoja huo zikiwa ni wanachama wa kundi la 4+1, pamoja na kutambua kuwa siasa za Marekani dhidi ya Iran zimegonga mwamba, lakini kivitendo badala ya kuiwekea mashinikizo Washington ili ibadilishe siasa zake kuhusiana na Iran, kiuhalisia zinaamiliana na Tehran kwa namna inavyotaka Marekani. Kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran, nchi hizo hazijaweza kuchukua hatua athirifu kwa ajili ya kupunguza athari hasi za vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran hususan katika kutekeleza mfumo maalumu wa mabadilishano ya fedha kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Ulaya (INSTEX). Katika radiamali yake kwa siasa hizo legevu za Ulaya, Iran ilianza kupunguza utekezaji wa majukumu yake katika mapatano ya JCPOA. Kutoheshimu Marekani JCPOA na hatua za Trump za kuyapiga vita mapatano hayo ya nyuklia pamoja na nchi za Ulaya kuhalifu ahadi na utekelezaji wa majukumu yao, ndivyo vilivyoifanya Tehran ipunguze hatua kwa hatua utekelezaji wa majukumu yake katika JCPOA.

Mkabala na hilo, badala ya Umoja wa Ulaya kuchukua hatua chanya na za maana kuhusiana na Tehran, zimesalimu amri kwa mashinikizo ya Marekani na kuamua kutekeleza utaratibu wa kutatua tofauti ndani ya mapatano ya JCPOA. Hatua hiyo ya Ulaya ambayo imechukuliwa kwa lengo la kuifurahisha Marekani sio tu haijapongezwa na Washington yenyewe, bali imezidisha matakwa ya kiuchu aliyonayo Trump na kumfanya ashadidishe mashinikizo yake dhidi ya nchi za Ulaya. Baada ya mkutano wake wa kwanza kufanya na Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya Ursula von der Leyen huko nchini Uswisi, Trump alionyesha hamu ya kushirikiana na Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kufikia mapatano ya kibiashara, lakini wakati huo huo akaonya kuhusu uwezekano wa kuyatoza ushuru zaidi magari yanayoingzwa Marekani kutoka Ulaya iwapo mapatano hayo hayatafikiwa. Suala hilo linaonyesha kuwa hatua ya Umoja wa Ulaya ya kuitumikia Marekani sio tu haijawa na taathira yoyote ya kumfanya Trump aachane na mpango wake wa kuzidisha ushuru wa biashara kwa magari yanayoingizwa Marekani kutoka Ulaya, bali umezidi kumshajiisha kuweka mashinikizo zaidi dhidi ya nchi hizo. Mtazamo wa mwenendo wa Trump kuzihusu nchi kama China, Iran na Korea Kaskazini hadi nchi za Ulaya pamoja na Canada na Mexico unaonyesha kuwa lengo la rais huyo wa Marekani ni kuyalazimisha mataifa hayo kuifuata kibubusa Washington na kutii matakwa yake yote kupitia mashinikizo, tena bila Marekani kulipa gharama yoyote mbadala. Na katika hilo hakuna tofauti yoyote kati ya maadui, washindani, waitifaki na washirika wa Marekani.
Post a Comment