Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kuwa, Serikali ya nchi hiyo imejipanga kuhakikisha kuwa, uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu unakuwa wa amani, uhuru na haki.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo jana jioni katika Ikulu ya Dar es Salaam alipokutana na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini Tanzania na kueleza kwamba, wakati wa kufanyika uchaguzi huo utakapowadia nchi na taasisi mbalimbali zitakaribishwa Tanzania kushuhudia zoezi hilo..
Rais huyo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amebainisha kwamba, uchaguzi ni jambo muhimu, Serikali imejipanga kuandaa mazingira mazuri katika uchaguzi huo.
Aidha amesema kama ninavyomnukuu: “Oktoba mwaka huu wa 2020 nchi yetu itafanya uchaguzi mkuu, zoezi la uchaguzi ni muhimu kwa nchi yoyote inayofuata misingi demokrasia, Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu unafanyika katika mazingira ya amani, uhuru na haki.”
Licha ya kupongezwa kwa hatua mbalimbali za maendeleo zilizochukuliwa na serikali yake, zikiwemo za kustawisha miundomsingi ya kiuchumi na kupambana na ufisadi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anakosolewa kuwa anaminya na kukandamiza demokrasia sambamba na kuendesha kampeni ya kuua vyama vya upinzani katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Wanasiasa wa upinzani wanadai kuwa serikali ya sasa ya Ris Magufuli imeweka mazingira magumu ya kufanya mikutano ya kisiasa na kukandamiza demokrasia.
Aidha vyama vya upinzani vinalalamikia kile vinachokitaja kuwa, kuandamwa viongozi wao na kesi mbalimbali, hali ambayo inawafanya washindwe kufanya shughuli za kuimarisha vyama vyao kwani kila mara wapo mahakamani au magereza.
Post a Comment