Ethiopia inatarajia kuitisha uchaguzi wa Bunge Mei au Juni mwaka huu licha ya kuweko wasiwasi na hofu wa usalama na vifaa vya kuendeshea zoezi hilo.
Hakikisho hilo limetolewa na Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia katika mkutano wake na waandishi wa habari akiwa na mwenyeji wake Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini na kusisitiza kuwa, ratiba kamili ya uchaguzi huo itatolewa na Tume ya Uchaguzi.
Uchaguzi huo wa Bunge unatarajiwa kuwa wa kwanza chini ya uongozi wa mshindi huyo wa tuzo ya Nobel ambaye alichukua wadhifa wa Waziri Mkuu wa Ethiopia Aprili mwaka 2018.
Waziri Mkuu wa Ethiopia ameeleza kuwa nchi yake inakabiliwa na changamoto nyingi siyo vifaa vya uchaguzi tu, bali kuna changamoto nyingine kama za usalama na amani.
Aidha amewataka wananchi wa Ethiopia pamoja na vyama vya siasa vya nchi hiyo kusaidia ili uchaguzi huo ufanyike katika mazingira ya amani na demokrasia.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, vyama vya upinzani nchini Ethiopia vimetahadharisha kuhusiana na hatua yoyote ile inayolenga kuakhirisha uchaguzi huo wa Bunge.
Tangu alipochukua uongozi nchini Ethiopia, Abiy Ahmed amefanya mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kisiasa na kumletea sifa kubwa kieneo na kimataifa, ingawa mabadiliko hayo yamepelekea pia kuibuka machafuko katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.
Post a Comment