Idadi ya wanajeshi wa Marekani wanaouguza majeraha ya ubongo kufuatia shambulio la Iran dhidi ya wanajeshi wa Marekani katika kambi moja nchini Iraq mwezi Januari imefikia 109, kulingana na maafisa wa Marekani.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Marekani Jumanne ya leo imesema kuwa, askari 109 wa nchi hiyo wamepatiwa matibabu kutokana na matatizo ya ubongo, ambapo wameongezeka askari 59 kwenye idadi ya awali.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Pentagon, askari 76 wamepatiwa matibabu na kurejea mahala pao pa kazi.
Imeendelea kufafanua kuwa askari 75 miongoni mwao wamepatiwa matibabu nchini Iraq, huku mmoja akitibiwa nchini Ujerumani.
Katika kutekeleza ahadi yake ya kulipiza kisasi kwa Marekani kutokana na nchi hiyo kumuua Luteni Jenerali Qassem Soleimani na wengine aliokuwa nao, Iran ilishambulia kwa makombora kambi ya kijeshi ya askari wa Marekani ya Ain Assad nchini Iraq hapo tarehe 8 Januari mwaka huu.
Licha ya Trump kudai kuwa katika shambulizi hilo hakuna askari aliyeuawa wala kujeruhiwa, lakini Washington imeendelea kukiri taratibu juu ya askari wake wengi kujeruhiwa.
Post a Comment