NA WAANDISHI WETU, MWANZA,SIMIYU.
WAZIRI mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kasim Majaliwa ameombwa kuingilia kati suala la kituo cha Mary Mother of God Center cha Lamadi, Busega kinacholea na kuhifadhi watoto wenye Ualbino kufuatia kuendeshwa bila vibali vya kusajiliwa huku akilindwa na kiongozi wa juu wa mkoa huo wa Simiyu.
Baadhi ya viongozi na wadau wamesema kuwa, Waziri Mkuu Majaliwa ndio pekee anaweza kuchukua hatua kwani mmiliki huyo mwanamama amekuwa akikahidi maagizo ya viongozi wa chini wa Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya na hata maafisa wa Ustawi wa Jamii na vyama vya watu wenye Ualbino.
Kituo hicho kipo Kata ya Lamadi kijiji cha Lamadi Kitongoji cha Itongo, kilianzishwa 2010 na mama mmiliki kwa lengo ya kukaa na watoto na wakati huo licha ya kushauliwa asajili amekuwa akipinga.
Imeelezwa Mama huyo mmiliki amekuwa akikitumia kwa njia ya kujipatia fedha kwa mgongo wa watoto wenye Ualbino kwa kukusanya misaada kutoka nje ya nchi na ndani huku watoto hao wakiishia kuvishwa nguo na kula chakula kinacholetwa na walezi/ wazazi wa watoto hao.
Pia amekuwa akiwatumikisha wafanyakazi pasipo kuwalipa na wakimdai anawatishia kuwabambikizia kesi.
"Amekuwa akiwafanyisha kazi watumishi lakini hawalipi mishahara na wakidai anawatishia kwamba walitaka kuiba watoto kituoni hapo.
Hadi sasa ana kesi nyingi na watumishi wake. Zingine zimepelekea kukamatiwa gari lake kwa amri ya mahakama" kilieleza chanzo cha taarifa kutoka makao makao makuu ya Busega.
Chanzo hicho kiliendelea kueleza kuwa;
Mama huyo amekuwa anawazuia watoto kujumuika na watoto wengine wakiwa shuleni hata vyakula vya shuleni amewazuia kula akitaka mgao wa vyakula hivyo upelekwe kituoni kwake.
"Kuna chakula Serikali inatoa kwa ajiri ya shule maalum lakini huyo mama anawazuia watoto hao kula chakula hicho pia hata hao watoto kwenda kukaguliwa ngozi zao kuona kama wanakansa huwa anawazuia kwenda hata kama ni maagizo ya Serikali hataki kuona hao watoto wakiwa karibu na watu wengine maana anaogopa kutoa siri za kituo wanavyo teswa.
Kuna mtoto alifia pale kituoni kwasababu ya kiburi cha huyo mama badala ya kumpeleka hospitalini analazimisha watoto wenzake kumuombea mgonjwa tunaomba Serikali isaidie hawa watoto na mtu sahihi kwa sasa ni Waziri Mkuu kwa maana anaweza kudili na huyu kiongozi wa juu wa mkoa anayemlinda " kilieleza chanzo cha taarifa kutoka Busega makao makuu ya wilaya hiyo.
Kiburi na jeuri ya mama huyo Mmiliki amekuwa akizuia watu kuishia nje ya geti viongozo wa serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya hiyo ya Busega na hata viongozi wa watu wenye ualbino wanaofika kituoni hapo kutokana na kukingiwa kifua na kiongozi wa juu wa mkoa huo wa Simiyu.
Chanzo kingine kilieleza kuwa, mama huyo amekuwa akiwatishia watendaji wa Serikali kuwa endapo atakifunga kituo hicho majengo hayo anaweza kugeuza hospitali hivyo hatishiki na abaendelea na shughuli zake.
Dulu za ndani kutoka kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya watu wenye Ualbino Kanda ya Ziwa pamoja na maafisa wa Ustawi wa Jamii walieleza kuwa, muda mrefu wamejaribu kumtaka mmiliki wa kituo hicho kuchukua hatua ya kukifunga kutokana na kukiendesha kinyume na utaratibu, ambapo ameshindwa kufanya hivyo na hata wakihoji wanaambiwa wamuone kiongozi huyo wa mkoa wa Simiyu.
"Tumeshapitia maadhimio mballimbali ya kuchukua hatua moja wapo ni la kukifunga kile kituo. Lakini hakufanya hivyo na anaendelea kujipatia fedha na mambo mengine kwa mgongo wa watoto wenye Ualbino.
"Wakati fulani alifika Waziri Possi wakati ule ni Naibu waziri wa walemavu alimuagiza kukifunga lakini hakufanya hivyo lakini pia jumuiko la asasi tulikaa kule Busega na ripoti ikaonesha kituo kile kifungiwe lakini hadi leo imeshindikana. Kwa sasa tunaiomba Serikali kuchukua hatua.
"Hii nchi inaendeshwa kwa sheria. Iweje aendeshe kituo kama hiki ndani ya nchi na hana vibali? Lakini tunahoji kwa nini analindwa hivi na viongozi wa mkoa? Anaishi na watoto wetu wenye ualbino lile jumba hakuna anayeingia ndani sisi wenyewe tunaishia nje hatufungulii geti licha ya kuwa ni wenye ualbino kwa maana hatuamini? Lakini hapohapo kuna watu wanaingia mule ndani watoto wale wanaamshwa usiku wanawaimbia na kucheza wazungu usiku wa manane" kilieleza chanzo.
Tunaomba Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Waziri wa mambo ya ndani Simba Chawene na watu wa Usalama watume watu wachunguze hiki kituo kwa sasa hatuna imani tena hata kama ni kuwasaidia watoto basi huku tofauti" kilieleza.
Kwa upande wake mdau wa masuala ya watu wenye Ualbino Kanda ya ziwa ambaye alishahi kufanya utafiti juu ya kituo hicho ambapo alikili kutopata ushirikiano kutoka kwa mmiliki huyo, mwenye ofisi zake Mjini Shinyanga, Elgeless Gaduzwe alisema:
" Tuhuma zinazofanyika katika kile kituo ni nyingi. Baadhi watoto wanasema wenyewe naomba serikali ikichukulie hatua stahiki.
Watoto wanateswa na yupo mmoja alivunjwa mguu akaondolewa kituoni na yule mmiliki.
Yaani ukifanya jambo lisilompendeza anakufukuza kituoni. Kuna watoto wenye ualbino wapo wengi mtaani amewafukuza" alieleza Gaduzwe.
Hata taarifa ambazo zimeweza kupatikana kwa wingi ni suala la viongozi wa serikali na vyama vya wenye ualbino kutoruhusiwa kuingia ndani ya kituo pamoja na suala la kuwaimbisha watoto usiku kucha kinyume taratibu.
Imaelezwa kuwa, Watoto hao uamshwa usiku na kulazimishwa kuimba nyimbo endapo wageni wapo kituoni hapo sanasana raia wa kigeni (wazungu ).
"Kumekuwa na mambo mengi ya ajabu. Lakini pia zimekuwepo 'kesi' watoto kupata mimba ndani ya kituo. Hizo mimba wanazipata wapi? Uchunguzi wetu umebaini ni wageni anaowaingiza mule ndani inasemekana wqpo wanaolala na wale watoto ambao wengine ni mabinti wakubwa" kilieleza chanzo hicho.
Pia licha ya kuwa, amejitolea kuwalea hao watoto, imebainika kuwa, mmiliki huyo amekuwa akiwatesa watoto hao na hata wakati mwingine kuwalazimisha kufanya kile ambacho hakikustahiri.
"Kuna watoto wanalazimishwa kwenda kanisani hata kama sio dhehebu lao.
Amewakataza hata kanisani wasiongee na mtu wala kukaa na watoto wengine." Kilieleza chanzo hicho.
Kwa upande wa chanzo kingine kutoka shule ya msingi Itongo ambayo ina wanafunzi maalum mbalimbali wakiwemo watoto hao wa wakituo cha mama huyo zilieleza kuwa watoto hao wamekatazwa kula chakula shuleni hapo.
"Malezi na mafundisho ya yule mama kwa Watoto hawa ni mabaya sana.
Hatusemi kumsingizia. Hata watoto tukiwabana wanasema wanavyofanyiwa. Imefika wakati chakula hapa shule cha serikali kwa ajili yao hawakitumii kwani aliwakataza kabisa" alieleza mmoja wa wawili ambaye anafundisha watoto hao (hakuwa tayari kutaja jina lake).
Pia imeelezwa kuwa, watoto hao wamekuwa na wakati mgumu kutokana na kuwatumikisha pasipokufuata misingi.
"Watoto alfajili wanaenda Ziwani pekee yao kuchota maji.
Pia wanakwenda pekee yao shuleni na kurudi ni Mungu tu ndie anayewalinda. Wazazi wamekuwa wakiogopa kusema kwa maana kuwa wamepunguziwa mzigo wa kuwalea hawa watoto" kilieleza chanzo hicho.
"Hawa watoto hawaruhusiwi kuongea wala kushikamana na watu wengine. Imefika hatua hata sisi walimu hapa Itongo tumekuwa na wakati mgumu na tunazitaarifu mamlaka husika nadhani ifuatiliwe huko" kilieleza chanzo.
"Watoto wanasinzia wakiwa darasani tukiwaliza kwanini wanasinzia majibu wanaeleza hawalali wanaimba na kusali hadi saa kumi ndipo huenda kulala.
"Pia wameeleza kuwa, wanadekishwa kwenye vyoo kwa mikono wakiwa wamesimamiwa na mama mmiliki na wanasema "anatukataza kumwambia MTU".
Mwalimu alimnukuu mmoja wa watoto hao; " tunakula makande ya ambayo yamechacha bahati mbaya tumbo likimshika mtoto akajinyea usiku unapigwa sana na kushikishwa kinyesi kwa mikono lakini pia wazazi wetu wakija kutusalimia wananyanyaswa sana wanakalishwa juani wakati mwingine mzazi mmoja aliwahi kumwagiwa maji na mama sister mbele yetu. Walisema hao watoto" alieleza mwalimu wa Itongo alipomnukuu mmoja wa wanafunzi hao.
" Kila mtoto anayelelewa analazimishwa mlezi ama mzazi kupeleka debe la chakula kati ya mahindi mchele ama unga. Na usipofanya hivyo mwanao anafukuzwa ama mzazi kutopata ruhusa ya kwenda kumuona mwanae" kilieleza chanzo hicho.
Kiliendelea kueleza;
"Wanapiga picha watoto wanatumia wazungu nje. Wanaleta misaada mbalimbali ikiwemo ya ndani na ya nje ya nchi lakini hadi leo hajasajiliwa kwa nini? Ni kwamba anahujumu uchumi. Lazima serikali iingilie kati: ilieleza taarifa ya chanzo hicho.
Hata hivyo baadhi ya mambo yaliyobainika imeelezwa kuwa, licha ya kutuo hicho mama huyo mmiliki kuanzisha 2010, tayari kina benki akaunti huku pia akiwa na wafanyakazi mbalimbali huku wengi wa wafanyakazi hao akigombana nao na wengine kuwafungulia kesi hizo.
"Anakaunti benki ya CRDB lakini pia kuna wafadhili wanamfadhili ikiwemo nchi moja ya Ulaya.
Fujo zake na hulka zake kila mtu anazijua lakini anakula na watu wengi ndio maana hachukuliwi hatua stahiki za kisheria." Kilieleza chanzo.
"Kuna mwanahabari wa Shinyanga na sasa yupo Simiyu huyu alikuwa anafanya kazi pale lakini kilichomkuta hatosahau na sasa amesamehe ikiwemo fedha zake kwa mama huyo kwani walipelekana hadi mahakamani" kilieleza chanzo.
Pia inaelezwa kuwa kutokana na kukingiwa kifua na kiongozi huyo wa mkoa ambaye amekuwa kipenzi cha Watanzania wengi kutokana na utendaji wake wa kazi ndani ya Simiyu, waau hao wameeleza kuwa huenda ikamchafua na ikapoteza taswira yake kwa jamii.
"Huyu mama anajiita Mtawa. Lakini fujo zake ni balaa. Ameshafanya fujo kanisani pale Lamadi.
Anaijua pesa zaidi na kutokana na hali hii anapata pesa nyingi sana lakini hatuoni maendeleo kituo kinaendeshwa kienyeji wanahabari wakipewa taarifa wanaenda kuchukua pesa wanakaa kimya" kilieleza chanzo.
"Inafika wakati mwandishi wa habari akienda kufuatilia mambo yanayoendelea akiona uendani na mipango yake anakutishia Polisi.
Wanahabari wengi licha ya kujua madudu ya huyu mama mmiliki lakini hawajachukua hatua hata ya kuandika. Kwa sasa serikali ichukue ili jambo kwa hatua hata huyu kigogo nae kwa namna anavuomlea itafika mahala atakuja kuingizwa matatani na huyu mama" kilimalizia chanzo hicho cha habari.
Waandishi wa habari hizi walimtafuta mama mmiliki huyo kujibu tuhuma zinazomkabiri ambapo simu zake ziliita bila mafanikio.
Naye afisa ustawi wa jamii Busea jana na leo licha ya kutafutwa kwenye simu hakuweza kupatikana.
Mwandishi wa habari hizi amepiga kambi ndani ya Mji wa Lamadi kwa siku kadhaa akifuatilia mwenendo wa shutuma hizo na tutawaletea upande wa pili kwa wanaoshutumiwa.
Fuatilia lipoti maalum ya mwendelezo wa shutuma za mmiliki wa kituo hicho sehemu ya pili.
Imeandaliwa na Samson Manyilizu na Shaban Ndelukela. (MWANZA, Bariadi).
Post a Comment