Viongozi wa mataifa ya Afrika wamekusanyika katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, kwa mkutano wa kilele wa 33 wa Umoja huo, unaolenga kujadili masuala ya usalama, huku suala la mgogoro wa Libya likitarajiwa kuchukuwa nafasi ya juu.
Katika mkutano huo, Afrika Kusini itachukua rasmi urais wa kupokezana kutoka kwa Misri.
Mkutano huo wa siku mbili unafanyika chini ya kauli mbiu ya "kunyamazisha risasi" inayoangazia malengo ya Umoja huo kufikia mwaka 2063.
Mpango huo ulioanzishwa mwaka 2013 unanuiwa kuyabadilisha mataifa ya Afrika na pia kupatikana kwa usalama na amani kote barani humo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anatarajiwa kuhudhuria mkutano huo utakaozungumzia mgogoro wa Libya.
Siku ya Alhamisi, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani alikutana na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini na kusisitiza umuhimu wa mataifa ya Afrika kujihusisha katika kuupatia suluhu ya kudumu mgogoro wa Libya.
Post a Comment