Ofisa mtendaji wa Kata ya Igunga, Robert Mwagala amewataja waliofariki dunia ni Dotho Joshua na Kulwa Joshua (13) wanaosoma darasa la sita shule ya msingi Makomelo na watatu ni Veronika Joshua (8) ambaye pia anasoma darasa la pili katika shule hiyo.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Februari 9, 2020, Mwagala amesema tukio hilo limetokea jana Saa 11:00 jioni kwenye bwawa hilo ambalo liko jirani na makazi yao.
“Wakati wakiogelea mmoja alizama wenzake wakaamua kumfuata kwa ajili ya kumuokoa, lakini nao walizama katika kina kirefu huku wakiomba msaada kuokolewa ndipo wananchi walifika na kufanikiwa kuwatoa lakini walikuwa tayari wamekunywa maji mengi,” amesema.
Amesema baada ya kuwatoa kwenye maji waliwapeleka hospitali ya Wilaya ya Igunga na wakati wakiendelea na matibabu, Saa moja usiku wote walifariki dunia.
Mzazi wa watoto hao, Joshua Said amesema wakati tukio hilo linatokea alikuwa Kijiji cha Malendi wilayani Iramba, Kiomboi, alipigiwa simu na majirani wakimtaarifu kuwa wanawe watatu wamezama kwenye maji na tayari wananchi wamewatoa na wamewawahisha hospitalini.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Mashaka Lunyilija alithibitisha kupokea watoto hao wakiwa taabani walipoteza maisha walipokuwa wakiendelea kutibiwa.
Miili ya watoto hao imeshakabidhiwa kwa wazazi wao kwa ajili ya maziko
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Barnabas Mwakalukwa alisema bado hajapokea taarifa hiyo kutoka kwa OCD Igunga, huku akiwataka wananchi kuwazuia na kuwalinda watoto wao wasicheze jirani ya visima na kwenye madimbwi ili kuepuka madhara yakiwamo ya vifo.
Amesema hadi sasa zaidi ya watoto 20 wameripotiwa kufa maji mkoani humo.
Post a Comment