Makumi ya watu wameuawa katika shambulizi la watu waliojizatiti kwa silaha katika jimbo la Katsina, kaskazini magharibi mwa Nigeria.
Sanusi Buba, Kamishna wa Polisi katika jimbo hilo amethibitisha habari za mauaji hayo, lakini amebainisha kuwa vyombo vya usalama vimeanzisha uchunguzi ili kuwatambua na kuwafikisha mbele ya sheria wahusika wa jinai hiyo.
Hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na shambulizi hilo, ingawaje kundi la kigaidi la Boko Haram na magenge mengine ya kitakfiri yenye mfungamano na Daesh (ISIS) yamekuwa wakifanya ukatili wa namna hii katika nchi za magharibi mwa Afrika.
Inaarifiwa kuwa, watu hao waliokuwa wamebeba silaha huku wakiwa juu ya pikipiki walishambulia vijiji vya Dankar na Tsauwa usiku wa kuamkia jana Jumamosi, ambapo wanavijiji 21 waliuawa kwa kuteketezwa kwa moto huku 9 wakiuawa kwa kupigwa risasi.
Hii ni katika hali ambayo, usiku wa Februari 9, watu wengine 30 waliuawa huku makumi ya wengine wakijeruhiwa katika shambulizi la kigaidi katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria, mwezi mmoja baada ya watu wengine 30 kuuawa kwenye mripuko wa bomu uliotokea karibu na daraja lenye shughuli nyingi katika jimbo hilo. Boko Haram ilikiri kutekeleza mashambulizi hayo mawili.
Wimbi hili la mashambulizi ya kigaidi linaonekana kuwa la ulipizaji kisasi haswa kwa kuzingatia kuwa, hivi karibuni, magaidi 250 wa kundi la kigaidi la Boko Haram waliuawa katika shambulizi la anga lililofanywa na jeshi la Nigeria katika misitu ya Kuduru jimbo la Kaduna
Post a Comment