Benki ya NMB inayoongoza kwa faida kubwa nchini, imeahidi kutumia bidhaa na huduma zake kuzisaidia serikali za mitaa kufikia malengo yake ya maendeleo na kuchangia ukuaji wa uchumi.
Ikiwa tayari imefikisha huduma za kibenki kwa zaidi ya asilimia 99 ya wilaya zote nchini kupitia mtandao wa matawi 224, zaidi ya ATM 800 na NMB Wakala, inayoifanya NMB iweze kutoa huduma za kibenki kwa serikali za mitaa ziweze kutekeleza na kusukuma mbele agenda ya maendeleo.
Ikiwa na umiliki wa soko wa asilimia 22 kwenye utoaji wa mikopo na amana za wateja kunaifanya NMB kuwa Benki inayoongoza nchini kwa kupata faida kubwa.
Kwa mfano, mwaka jana NMB ilipata faida ya shilingi bilioni 148.6, ikiwa ni ongezeko la asilimia 52 ikilinganishwa na faida ya shilingi bilioni 97.7 iliyopatikana mwaka uliotangulia. Kwa upande wa mikopo, NMB ilitoa shilingi trilioni 3.61, ikiwa ni ongezeko la asilimia 12 ukilinganisha na shilingi trilioni 3.27 zilizokopeshwa Mwaka 2018.
Hayo yalielezwa mwisho wa wiki katika hafla fupi iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala - Sophia Mjema, ikiwakutanisha wafanyakazi wa manispaa na wafanyakazi wa Benki ya NMB.
Akiongea katika hafla hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Biashara za Serikali wa NMB - Vicky Bishubo, amesema Benki ya NMB imejidhatiti kuendelea kufanya kazi na serikali za mitaa katika kusukuma mbele miradi mbalimbali yenye lengo la kuboresha Maisha ya watu.
“Tunafanya kazi na Manispaa na Halmashauri mbalimbali katika maeneo ya ukusanyaji mapato ya serikali, kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo wadogo na wa kati, wafanyakazi wa serikali, na kupitia sera ya Benki ya majukumu ya kijamii kwa kusaidia huduma za elimu, afya na majanga mbalimbali,” alisema.
Kwa mfano, Benki ya NMB mwaka jana ilitoa zaidi ya dhamana 500 kwa wakandarasi wazawa ili kuwawezesha kugharimia miradi mbalimbali ya ujenzi nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bi. Mjema aliwataka wafanyakazi wa manispaa na wananchi wote wa Wilaya hiyo kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Benki ya NMB katika kuendeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi na nyingine kama mikopo ya nyumba.
Naye Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam -Badru Idd alisema kwa miaka yote Benki ya NMB imekuwa ikitumia rasilimali na juhudi zake kutoa huduma za kibenki kuwafikia wale ambao bado hawajapata huduma za kibenki hasa wale wa vijijini.
#NMBKaribuYako
Mkuu wa Wilaya ya Ilala - Sophia Mjema akizungumza wakati wa ushiriki wa kifungua kinywa cha pamoja na wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Benki ya NMB uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mkoa wa Dar es Salaam. Kutoka kushoto kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ilala - Jumanne Shauri, Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam - Badru Iddi, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Serikali wa NMB - Vicky Bishubo na Katibu Tawala wa Manispaa ya Ilala - Charagwa Selemani.
Wakipata kifungua kinywa.
Wakiwa katika picha ya pamoja.
Post a Comment