Michuzi Blogu imefanya uchunguzi wake katika masoko ya Sabasaba na Majengo ambapo wafanyabiashara kadhaa wameitaja mvua kama chanzo cha mfumuko wa bei ya zao hilo muhimu kwenye mapishi.
Tofauti na kuwa kiungo cha mboga zao hilo pia hutumika kutengenezea kachumbari na 'tomato sauce' vyote hivyo ni katika kuleta ladha ya mapishi na kuongeza ubora wa chakula.
Katika mahojiano hayo Wafanyabiashara hao wamesema kwa sasa bei ya nyanya imekuwa ni ghali sana na sababu kubwa ya kupanda kwa zao hilo imetokana na mvua kubwa ambazo zimekua zikinyeesha kwa muda mrefu nchini.
" Hizi mvua zinazonyeesha ndiyo zimechangia kupanda kwa bei ya nyanya ambapo sasa Boksi la Kilo 40 ambalo kawaida tumekua tukilinunua kwa Sh 40,000 kwa sasa limepanda na kuwa Sh 97,000 hadi Laki Moja hivyo imetulazimu sisi kuuza kutokana na tunavyonunua kwa wakulima," Amesema Bi Khadija Abdallah ambaye ni mfanyabiashara soko la Majengo.
Kwa upande wake Pili Mushi ambaye anajishughulisha na uuzaji wa mihogo ya kukaanga amesema kupanda huko kwa nyanya kumeathiri kwa kiasi kikubwa biashara yake katika kwani nyanya amekua akizitumia kutengeneza Pilipili na kachumbari kwa ajili ya wateja wake.
" Kwa kweli nyanya zimepanda kwa kiasi kikubwa sana, mwanzoni tulikua tunanunua sado kwa Sh 3,000 hadi 4,000 sasa hivi sado imepanda hadi Sh 10,000. Kwa sisi wafanyabiashara wadogo mfumuko huu umetuathiri sana," Amesema Pili.
Awali kabla ya mfumuko huo nyanya tano ndogondogo zilikua zikipatikana hadi kwa Sh 500 wakati zile kubwa zikiuzwa tano Sh 1,000 lakini hivi sasa nyanya moja ni Sh 500.
Changamoto hiyo imewakumba hadi Mama Ntilie ambao wametoa kilio chao wakiitaka serikali kuingilia kati kwani inawakwamisha katika biashara zao.
" Hii hali ilianza kama utani lakini kwa kweli imekua mbaya kadri siku zinavyozidi kwenda mbele. Sasa hatuelewi ni mvua inasababisha huu mfumuko au ni nini," Amesema mmoja wa Mama Ntilie wa Soko la Majengo.
Nae Afisa Masoko wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, James Yuna amesema kwa kipindi hiki mfumuko wa Bei ya nyanya umekuwa ni mkubwa na kuwataka wafanyabiashara na watumiaji wa zao hilo kuwa watulivu wakati huu ambao halmashauri ya Jiji inapotafuta njia bora ya kuondoa mfumuko huo ili kuweza kuleta unafuu kwa upande zote mbili.
" Tunafahamu kuwepo kwa changamoto hii na hakika ni jambo linalotuumiza kichwa, lakini niseme tu kwamba tunafikiria njia bora ya kutatua ambayo itakua na manufaa kwa watumiaji wa nyanya na wafanyabiashara kwa ujumla," Amesema Yuna.
Post a Comment