Featured

    Featured Posts

RAIS DK. MAGUFULI ASHANGAZWA NA VIONGOZI WA MKOA WA DAR ES SALAAM KUTOTENGA FEDHA ZA KUBORESHA BARABAR5A ZA KIGAMBONI CHINI YA MRADI WA DMDP

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli akiongozana  na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Sarah Msafiri
na viongozi wengine wa ngazi mblimbali baada ya kuzindua jengo la Mkuu wa Wilaya hiyo ikiwa ni sehemu ya uzinduzi rasmi wa Wilaya hiyo ya Kigamboni alioufanya Rais Magufuli, leo
 Jumanne Februari 11, 2020. (Picha na Ikulu)
KWA PICHA NYINGINE NYINGI ZA TUKIO HILO, TAFADHALI >>>BOFYA HAPA


KIGAMBONI, Dar es Salaam
Rais Magufuli ameelezea kushangazwa kwake na kitendo cha viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kutotenga fedha za kuboresha  barabara za Kigamboni chini ya Mradi wa Maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP), hivyo kuagiza fedha za mfuko wa barabara zilizotengwa kwa ajili ya wilaya zilizonufaika na mradi huo wa DMDP zipelekwe Kigamboni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara ya lami ya mzunguko ya Kimbiji – Mjimwema.

Rais Dk. John Magufuli, amesema hayo leo wakati akizindua rasmi Wilaya ya Kigamboni Mkoani Dar es Salaam, jengo jipya la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo na jengo la Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni na majengo mawili ambayo ni la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo na la Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni.

Akiendelea na hotuba yake, Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenister Mhagama na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) William Erio kuchukua hatua dhidi ya mkandarasi aliyepewa zabuni ya kujenga kipande cha barabara cha kuunganisha na Daraja la Nyerere (Kigamboni) kutokana na mkandarasi huyo kupanga gharama kubwa za ujenzi kupita kiasi. 

Rais Magufuli ametoa wiki moja kwa watumishi wa Wilaya ya Kigamboni hasa wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama kuhamia Kigamboni ikiwemo kuhamia katika majengo ya NSSF ambayo hayakaliwi na watu, badala ya kuishi katika wilaya zingine za Mkoa wa Dar es Salaam na pia ameiagiza TAMISEMI kutoa sh. Bilioni 2 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa nyumba za watumishi katika eneo la Serikali lilitolewa kwa Manispaa hiyo kutoka NAFCO.

Rais magufuli ameagiza viongozi wa Kigamboni kutatua tatizo la mwekezaji ambaye anazuia wananchi kupita katika eneo lake wanapokwenda kuvua samaki ama mazikoni na ameonya kuwa akiendelea hivyo hatosita kufuta hati miliki ya mwekezaji huyo.

Wilaya ya Kigamboni yenye eneo la kilometa za mraba 577.9 (hekta 57,786.8) ilianzishwa kwa tangazo la Serikali namba 462 la mwaka 2015 ikimegwa kutoka Wilaya ya Temeke kwa lengo la kusogeza karibu huduma kwa wananchi.

Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo lenye ukubwa wa meta za mraba 1,285, ambalo Rais Magufuli amelizindua leo, lina uwezo wa kuchukua watumishi 50 na ujenzi wake umegharimu sh. Bilioni 1.6 wakati jengo la Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni lenye ukubwa wa meta za mraba 7,342, lina uwezo wa kuchukua watumishi 450 ujenzi wake ukiwa umegharimu sh. Bilioni 5.2.

Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Kigamboni kwa kusogezewa huduma za utawala na pia amewapongeza viongozi wa Kigamboni wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Sara Msafiri na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kujenga majengo hayo vizuri.

Ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha wilaya hiyo kwa kuhakikisha miundombinu inaimarishwa ambapo ametoa wiki moja kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kukabidhi eneo lote la ekari 719 (lililokuwa likimilikiwa na Shirika la Taifa la Kilimo na Chakula - NAFCO) kwa Wilaya ya Kigamboni ili wilaya hiyo iliendeleze kwa kujenga majengo ya umma zikiwemo nyumba za watumishi.

Akizungumzia mvua zinazoendelea kunyesha Rais Magufuli amewatahadhalisha Watanzania kutojenga makazi katika maeneo ya mabondeni na badala yake watumie mabonde na maji ya mvua zinazonyesha kwa kilimo badala ya kubaki wakilalamika.

Aidha ametumia pia hafla hiyo kuagiza kufukuzwa kazi mara moja kwa Mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Daniel Maleki aliyeonekana katika video akikashifu na kuchana kitabu kitukufu cha Quran.

Baada ya kuzindua Wilaya ya Kigamboni, Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli, Waziri Jenister Mhagama, Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mussa Azzan Zungu ametembelea Bustani ya Wanyama ya Dar es Salaam (Dar es Salaam Zoo) ambapo pamoja kuwapongeza wawekezaji hao, ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kufuga wanyamapori ili waweze kunufaika na fursa hiyo muhimu.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana