Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Alhaji Juma Kilimba, akizungumza kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 43 ya chama hicho yaliyofanyika kimkoa Wilaya ya Singida Vijijini hivi karibuni. Wengine ni viongozi mbalimbali wa chama hicho na Serilikali na Wabunge. KWA PICHA ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 43 YA CCM >> BOFYA HAPA
Na Godwin Myovela, Singida
Baada ya mvutano mkubwa ambao umekuwepo baina ya madiwani, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na viongozi wa Serikali kuhusu wapi panastahili kujengwa Makao Makuu ya Halmashauri ya Singida, CCM mkoa wa Singida imetoa msimamo wake kwamba Ofisi hizo zitajengwa Ilongelo na sio kwingineko.
Akihutubia mamia wa wanachama wa CCM, kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 43 yaliyofanyika kimkoa wilaya ya Singida Vijijini hivi karibuni, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida, Alhaji Juma Kilimba alisema msimamo wa CCM ngazi ya mkoa huo kwamba ofisi hizo zitajengwa Ilongelo.
“Mnachotaka kukifanya ninyi madiwani hasara yake itakuwa ni kubwa sana, hatuhitaji tena kupoteza hiyo fedha inayotaka kutolewa, mara ya kwanza mlipoteza fedha ya ujenzi wa hospitali kwa sababu ya ubishi wa namna hii…heshimuni taratibu na maelekezo ya Chama, lazima tuheshimiane na tuwe na utaratibu wa kujenga nidhamu, “ alisema Kilimba
Akifafanua sababu ya kujengwa Ilongelo, alisema mwaka 2006 kulifanyika vikao kadhaa kuhusu jambo hilo na mambo mengine kadhaa ikiwemo kuzaliwa kwa wilaya za kiserikali za Ikungi na Mkalama, na mpaka sasa mukhtasari na maazimio yaliyofikiwa upo. Sasa kwa taratibu za vikao jambo lolote la kikao linaondolewa na kikao
Alisema kwa sasa kuna halmashauri mbili ambazo zipo chini ya Wilaya ya Singida Mjini, chini ya Mkuu wa Wilaya mmoja, kwa hiyo wakati wa vikao vile mchakato ulifanyika kwa mahali pake, na hakukuwa na mchakato ambao ulikuwa unabatilisha au kubadilisha maoni ya Ilongelo kuwa sehemu sahihi.
“Mnakumbuka kuhusu ujenzi wa hospitali eneo hili maneno yalikuwa mengi, lakini tunamshukuru Waziri Mkuu akaja akatoa majibu, na siku iliyofuata Mheshimiwa Rais akaagiza kwamba halmashauri zote ziende kwenye maeneo ya kazi, na Mkurugenzi wetu uyu ametekeleza hilo yupo hapa Ilongelo,” alisema
Kilimba alisema sababu ya madiwani hao kung’ang’ania ofisi kwenda huko njia panda ni kwamba wengi wao wamepatiwa viwanja vya kati ya heka 2 na 5 na tayari chama kimekwishaandika barua Takukuru ya kuwataka kuchunguza juu ya tuhuma hizo
“Kwani ofisi ya Mkurugenzi ina ukubwa gani? Kwamba eneo hili hakuna eneo na je mmeshawauliza wananchi wa Ilongelo kama hawana hilo eneo?,” alihoji huku akiwataka madiwani hao kutotazama maslahi yao badala yake wajikite katika muktadha wa mahitaji ya muda mrefu kwa ustawi wa watu wa Singida vijijini..lengo letu hasa ni kutaka kuharakisha ujenzi huu na hayo mengine yafuate baadaye,” alisema na kuongeza:
“Hata kama eneo mmeshalipata kigezo cha kuweka makao haya Merya kinakidhi? kuna hospitali, kuna kituo cha polisi, huduma za maji, umeme, barabara, shule, soko na huduma nyinginezo…huko mnakotaka kwenda serikali itaingia gharama kubwa kwa sasa, lengo letu hasa ni kutaka kuharakisha ujenzi huu na hayo mengine yafuate baadaye,” alisema Kilimba.
CCM mkoani hapa kimeadhimisha miaka 43 kwa mafanikio makubwa, ikiwemo juhudi zinazoendelea za kukarabati uwanja wake wa Liti ambao huko nyuma ulijulikana kama Namfua, kujenga na kusimamia nidhamu, kujenga ofisi zake mbalimbali ikiwemo ofisi yake ya wilaya singida DC.
Aidha, katika maadhimisho hayo shughuli mbalimbali zilifanyika ikiwemo kupanda miti, kutembelea watoto wa makundi maalumu na kuwakabidhi zawadi mbalimbali sanjari na wanachama na wabunge kadhaa wa mkoa huo kuchangia ujenzi wa ofisi ya chama hicho unaoendelea.
Post a Comment