Featured

    Featured Posts

WAZIRI MKUU AAGIZA WADAIWA WOTE NHC WALIPE MADENI KABLA YA MEI 30

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) uwaandikie barua wapangaji wote wanaodaiwa kodi na shirika hilo na wahakikishe zimelipwa ifikapo Mei 30, mwaka huu.

“Orodha ya wadaiwa niliyonayo hapa ni kubwa na wengine inaonesha wamehama na wameondoka bila kumalizia kodi zao. Hawa wote ni lazima tuwafuatilie na walipe madeni yao,” amesema.

Ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Februari 11, 2020) wakati akizungumza na viongozi na wajumbe wa Bodi ya shirika hilo kwenye kikao kilichofanyika ofisini kwake, Magogoni, jijini Dar es Salaam.

“Taasisi zote za Serikali ambazo zimepanga kwenye nyumba za shirika ni lazima zilipe madeni. Chombo chochote cha Serikali kinaishi na bajeti, kwa hiyo hata kama wamejenga ya kwao, walipaswa walipe kabla hajahama.”

“Waandikieni barua wadaiwa wote ili walipe. Tunaelekea mwishoni mwa bajeti ya mwaka huu, na hawa wote wawe wamelipa ifikapo tarehe 30 Mei, 2020. Nami nipate orodha ya taasisi za Serikali zinazodaiwa ili niwafuatilie; nitawaita Makatibu Wakuu wao mmojammoja. Hao wadaiwa binafsi wachukulieni hatua stahiki,” amesisitiza.

Waziri Mkuu amesema madeni ambayo taasisi za Serikali zinadaiwa yanafikia sh. bilioni 4.3 na kama zitalipwa zote hizo, zitalisaidia shirika kuendelea na mpango wake wa ujenzi wa nyumba nafuu kwenye maeneo mbalimbali.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amelitaka shirika hilo lijielekeze kwenye ujenzi wa nyumba bora na za bei nafuu kwa sababu mahitaji ya nyumba nchini bado ni makubwa. “Simamieni suala hili, ili tupate nyumba nzuri na za bei nafuu. Simamieni wataalamu wenu ili wasikadirie miradi ambayo bei zake zitakuwa juu sana na kisha wananchi wetu washindwe kumudu. Ni lazima mhakikishe kuwa wananchi wa kipato cha chini wananufaika na uwepo wa shirika,” amesema.

Amesema wataalamu hao wanahitaji kudhibitiwa kwa sababu sehemu kubwa ya malighafi inapatikana hapa nchini. “Hivi sasa kokoto, nondo, mabati na vifaa vingi vya ujenzi vinazalishwa hapa nchini, siyo kama zamani. Iweje bei ya kuuza nyumba inakuwa ya kutisha?” alihoji.

Pia Waziri Mkuu aliwataka viongozi hao waimarishe ukusanyaji wa mapato ya shirika hilo kwa kuhakikisha kodi zinakusanywa kwa njia ya kielektroniki. “Tuache tabia ya kuruhusu maafisa kwenda nyumba kwa nyumba na kudai shilingi 500,000 kwa risiti za kuandika. Tumieni control number, ili mwananchi aweze kulipia kwa simu au benki na hela inaingia moja kwa moja katika shirika,” amesema.

Mapema, akitoa taarifa ya shirika hilo mbele ya Waziri Mkuu, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dk. Sophia Kongele alisema shirika hilo linawadai wapangaji waliohama na waliopo ambao wengi wao ni wizara na taasisi za Serikali na akaomba wahimizwe kulipa ili wao waweze kuendesha shirika kwa ufanisi.

“Kwa wapangaji waliohama bila kulipa, shirika linadai shilingi bilioni 4.353 na kwa wapangaji waliopo wanadaiwa kiasi cha shilingi bilioni 1.286, na hivyo kufanya deni lote lifikie shilingi bilioni 5.641.”

Alisema shirika hilo limekuwa likiendesha miradi ya ndani na ya nje ikiwemo kutekeleza miradi ya ujenzi ya taasisi nyingine kama mkandarasi na mshauri. “Shirika limefanikiwa kumaliza miradi 16 ya ukandarasi yenye thamani ya shilingi bilioni 16.8 na linaendelea na ujenzi wa miradi 10 ya ukadarasi yenye thamani ya shilingi bilioni 69.4,” alisema.

Alisema wanaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi mikubwa ya Morocco Square, Seven Eleven (Kawe), Golden Premier Residence (Kawe) na Regent Estate ambayo kwa sasa imesimama kutokana na ukosefiu wa fedha.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana