Watu 20 wameaga dunia katika mkanyagano wa harakati za kutaka kukanyaga 'mafuta ya upako' kwenye kongamano la 'Mtume' Boniface Mwaiposa lililofanyika uwanja wa Majengo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, kaskazini mashariki mwa Tanzania jioni ya jana Jumamosi.
Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi , watu zaidi ya 40 walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi ya Mkoa wa Kilimanjaro baada ya kujeruhiwa kutokana na mkanyangano huo.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba ameliambia Mwananchi kuwa, "taarifa za awali tulizonao ni kuwa, waumini 20 wamepoteza maisha lakini tunaendelea kufuatilia maeneo mengine ya zahanati, vituo vya afya na hospitali kama kuna watu walipelekewa huko."
Duru za habari zinasema kuwa, yumkini idadi ya wahanga wa tukio hilo ikaongezeka kwa kuwa hakuna taarifa rasmi hadi sasa kuhusu idadi ya walioaga dunia na waliopelekwa katika hospitali na vituo vya afya vya mkoa huo.
Tukio hilo linatajwa kuwa baya zaidi kuwahi kuukumba Mkoa wa Kilimanjaro katika miaka ya hivi karibuni.
Post a Comment