Shirika la Afya duniani WHO limetoa tahadhari kwa nchi za ulimwengu kuandaa mikakati kabambe ya kukabiliana na ugonjwa huo iwapo utaenea na kuwaambukiza wakazi wake kwa kuzingatia kwamba mataifa zaidi yanaendelea kuripoti visa vya maambukizi.
Ujerumani, Australia, Japan, Korea Kusini, Falme za Kiarabu, Marekani na Vietnam zote zimeripoti maambukizi mapya mnamo siku ya Jumamosi huku Uhispania ikithibitisha maambukizi ya kwanza katika nchi hiyo. Ufilipino imetangaza kifo cha kwanza kutokana na homa inayosababishwa na virusi vya Corona.
Wakati huo huo, maafisa sita wamefukuzwa kazi katika mji wa Huanggang ulio jirani na mji wa Wuhan ambako ndiko virusi hivyo vilipoanzia. Kwa mujibu wa taarifa za shirika la habari la China Xinhua, maafisa hao wamefutwa kazi kutokana na utendaji kazi mbaya katika kushughulikia mlipuko wa virusi vya Corona tangu vilipozuka.
Licha ya kuonyesha dalili za kupungua maambukizi mapya, mamlaka ya mkoa wa Hubei imerefusha muda wa likizo ya mwaka mpya wa Lunar, iliyotarajiwa kumalizika mwisho wa wiki hii, hadi katika mwezi huu wa Februari. Msongamano wa mamilioni ya watu wanaosafiri wakati kama huu ambao wanarejea kutoka sehemu mbalimbali unaleta hofu ya uwezekano wa kusababisha maambukizo mapya. Mamlaka za miji katika mkoa wa Hubei zinawahimiza watu wote waepukane na mikusanyiko. Shule zote katika mkoa huo zimeahirisha kufunguliwa kwa muhula mpya hadi taarifa rasmi itakapotolewa.
Pamoja na kuweka vikwazo vikali vya usafiri nyumbani, China imekasirishwa na vikwazo vilivyowekwa na serikali za nje na imekosoa agizo la Marekani la kuwazuia kuingia nchini humo watu wasio raia wa Marekani ambao waliitembelea China katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.
China imesema mbali na kuiteremshia sifa ya kimataifa, hatua kama hiyo inaweza kuathiri zaidi uchumi wake wa ndani ambao kwa miongo kadhaa unakua kwa kiwango cha chini huku vita vya kibiashara kati yake na Marekani vikiwa bado kwa kiasi kikubwa havijapata suluhisho.
Mashirika ya ndege ya Canada, Lufthansa, shirika la ndege la Uingereza, Uturuki, Marekani, KLM, Air France, Qantas na Delta yamefuta mamia ya safari zake za ndege kwenda na kutoka China bara. Hatua hiyo inaiweka China katika hali ya kutengwa kutokana na kuongezeka kutokuwepo na shughuli za usafiri za kimataifa pamoja na kusimamishwa kwa safari za ndege.
Ujerumani, Uturuki na Marekani ni kati ya nchi ambazo zilipeleka ndege kuwaondoa raia wao kutoka mji wa Wuhan. India inajiandaa kuwaondoa raia wake wapato 250 kutoka mji wa Wuhan. Mapema wiki hii Urusi ilitangaza kufunga mpaka wake na China hatua sawa iliyochukuliwa na nchi zingine majirani wa China.
Vyanzo:/AP/DPA/RTRE
Post a Comment