Mahakama moja nchini Misri imewahukumu adhabu ya kifo watu 37 akiwemo Hisham al Ashmawy afisa wa zamani wa jeshi la nchi hiyo aliyejiunga na magenge ya kigaidi.
Ashmawy alitiwa mbaroni katika mji wa Derna wa mashariki mwa Libya mwishoni mwa mwaka 2018 na alikabidhiwa kwa maafisa wa Misri mwezi Mei mwaka jana.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Ashmawy amepatikana na hatia ya makosa mengi ikiwemo kufanya njama za shambulio lililotokea mwaka 2014 na kuua wanajeshi 22 wa Misri karibu na mpaka wa Libya na pia kuhusika katika jaribio la kumuua waziri wa mambo ya ndani wa Misri mwaka 2013.
Afisa huyo wa zamani wa jeshi la Misri alikuwa anaongoza kundi linalojiita Ansar Bayt al Maqdis ambalo ni moja ya makundi hatari nchini Misri na ambalo mwaka 2014 lilitangaza utiifu wake kwa genge la kigaidi la Daesh yaani ISIS.
Watu wengine 36 waliohukumiwa kifo pamoja na Ashmawy, nao wamepatikana na hatia ya makosa ya ugaidi.
Hukumu za watu hao amekabidhiwa Mufti Mkuu wa Misri ambaye kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, hukumu za kifo hupelekwa kwake kwanza kupata maoni yake kabla ya kutekelezwa.
Mwezi Novemba mwaka jana, mahakama moja ya kijeshi ilimuhukumu Ashmawy adhabu ya kifo kwa kosa jingine la kigaidi. Mahakama nyingine za Misri za kijeshi na kiraia nazo zimewahi kutoa hukumu za kifo cha Ashmawy akiwa hayupo mahakamani.
Post a Comment