Mratibu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Yemen, Lise Grande, amesema watu wengi wanauawa kwenye mashambulizi yasiyo na msingi nchini Yemen. Kwa mujibu wa sheria za kimataifa pande hasimu zilizo kwenye mizozo zinatakiwa kutoa kipaumbele katika kuwalinda raia. Grande amesema inashangaza kuwa hata baada ya miaka mitano ya mzozo wa Yemen pande zinazopigana zimeshindwa kuheshimu wajibu huo.
Shirika la Save the Children limelaani mashambulio hayo na kusema kwamba inaonyesha mzozo wa nchini Yemen hauna dalili ya kupungua. Shirika hilo limetaka uchunguzi huru na wa haraka ufanyike na kwamba wahusika wachukuliwe hatua za kisheria. Mkurugenzi wa Save the Children nchini Yemen Joubert Xavier ametoa wito wa kusimamisha uuzaji wa silaha kwa pande zinazopigana nchini Yemen.
Msemaji wa Wizara ya Afya iliyo chini ya waasi wa Houthi, Youssef al-Hadiri, ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kwamba wengi wa waliojeruhiwa ni wanawake na watoto. Al Hadiri ameulaumu muungano wa kijeshi unaongozwa na Saudi Arabia kwa kutatiza shughuli za uokoaji katika eneo kulipotokea mashambulio hayo na amearifu kwamba muungano huo unaendelea kufanya mashambulio ya ndege ingawa hakutoa maelezo zaidi.
Televisheni inayomilikiwa na waasi wa Houthi (al-Masirah) imeripoti juu ya kushambuliwa kwa mabomu umati wa watu ambao walikuwa wamekusanyika karibu na ndege ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia iliyodunguliwa na waasi hao katika eneo hilo siku iliyopita. Hakuna taarifa zozote kutoka upande wa muungano unaongozwa na Saudia.
Kushoto: Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Faisal bin Farhan Al Saud. Kilia: Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo.
Yemen imetumbukia kwenye machafuko kati ya serikali inayoungwa mkono na Saudi Arabia na kundi la waasi wa Houthi lenye mafungamano na Iran tangu mwaka 2014. Mzozo nchini humo umeongezeka tangu Machi mwaka 2015, pale Wahouthi walipouteka na kuuweka chini udhibiti wao mji mkuu wa muda wa serikali, Aden, hatua iliyosababisha Saudi Arabia na washirika wake wa Sunni kuanza operesheni ya mashambulio ya anga dhidi ya kundi la Washia. Mzozo huo umeitumbukiza Yemen katika baa la njaa na kuharibu mfumo wa afya katika nchi hiyo inayokabiliwa na umaskini.
Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia mwana mfalme Faisal Bin Farhan Al Saud amesema licha ya vurugu kuendelea kuongezeka nchini Yemen, Saudi Arabia imeazimia kuendelea na mazungumzo ya amani pamoja na waasi wa Houthi.
Mapigano ya Yemen yameingia katika mwaka wa tano tangu waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran walipoiondoa madarakani serikali ya aliyekuwa Rais wa Yemen Abd Rabbu Mansour Hadi, mwishoni mwa mwaka 2014.
Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia mara kwa mara umekosolewa kwa kusababisha idadi kubwa ya vifo vya raia kutokana na mashambulio yake ya mabomu, hadi kufikia baadhi ya serikali za Magharibi kusimamisha usafirishaji wa silaha katika Mashanchi zinazoshiriki katika vita vya Yemen. Wakati huo huo umoja huo umesema utawafungulia mashtaka wanajeshi wanaotuhumiwa kuhusika na mashambulio mabaya ya ndege dhidi ya raia wa Yemen.
Post a Comment