Tarehe tatu Januari mwaka huu wa 2020, rais wa Marekani, Donald Trump, alifanya jinai ya kutoa amri ya kuuliwa kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) na wanajihadi wenzake tisa karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad, huko Iraq.
Trump alijigamba kuwa ndiye aliyetoa amri ya kufanyika jinai hiyo kwa madai kuwa Luteni Jenerali Soleimani alikuwa ana mpango wa kushambulia taasisi muhimu za Marekani. Hata hivyo, ripoti rasmi iliyotolewa hivi sasa na ikulu ya Marekani (White House) inaonekana kukinzana waziwazi na madai hayo. Eliot Engel, Mkuu wa Kamati ya Masuala ya Nje ya Bunge la Wawakilishi la Marekani juzi Ijumaa alitangaza kupitia taarifa maalumu kwamba vipengee vya ripoti rasmi ya White House vinakinzana na madai yaliyotolewa na Donald Trump kwamba shambulio dhidi ya Luteni Jenerali Soleimani lilifanyika ili kuzuia kile alichokitaja kuwa kamanda huyo alikuwa amekaribia kuiletea madhara Marekani. Mbunge huyo wa ngazi ya juu katika Bunge la Wawakilishi la Marekani amesisitiza kuwa, katika ripoti ya White House hakujaashiriwa tishio lolote lililokuwa limekaribia sana kutokea yaani (Imminent Threat); na hiyo imedhihirisha wazi kwamba sababu za kuhalalisha shambulizi hilo zilizotolewa na Trump kwa wananchi wa Marekani si sahihi.
Mkuu wa Kamati ya Masuala ya Nje katika Bunge la Wawakilishi la Marekani aidha amekitaja kifungu cha sheria kilichotegemewa na Trump kuhalalisha shambulizi dhidi ya Luteni Jenerali Soleimani kuwa nacho si sahihi. Kabla ya kufichuliwa suala hilo, baadhi ya viongozi wa serikali ya Trump walisema kuwa shambulio la anga dhidi ya Luteni Jenerali Soleimani na wenzake lilifanyika kwa mujibu wa eti sheria iliyopasishwa mwaka 2002 ambayo ndiyo iliyoandaa uwanja wa kushambuliwa Iraq mwaka 2003. Engel anaamini kuwa, serikali ya Trump imetegemea kifungu hicho cha sheria ili kukwepa kutoa jibu kwa Kongresi kuhusu hatua yake hiyo. Engel amesema: Ili iweze kukwepa kusailiwa na kuitwa mbele ya Baraza la Kongresi kutoa maelezo kuhusu hatua yake hiyo, serikali ya Trump imedai kuwa Kongresi ilitoa kibali kwa shambulizi hilo kwa mujibu wa maazimio ya Iraq yaliyopasishwa mwaka 2002. Na ukweli ndio huo kwamba, kwa upande wa kisheria kisingizio hicho hakina maana yoyote. Sheria hiyo ilipasishwa mwaka 2002 ili kukabiliana na Saddam Hussein na haina mfungamano wowote na Iran au viongozi wa utawala wa Iran huko Iraq."
Luteni Jenerali Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds na Abu Mahdi al Muhandes Naibu Mkuu wa Harakati ya al Hashd al Sha'abi ya Iraq na wanajihadi wenzao wanane waliuliwa shahidi alfajiri ya Januari tatu mwaka katika shambulio la anga la wanajeshi vamizi na magaidi wa Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Bagdhdad. Kama ilvyotangazwa na Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon); Donald Trump ndiye aliyeamuru kufanywa jinai hiyo. Marekani ilisema kuwa imefanya jinai hiyo kutokana na eti Kamanda Soleimani aliwasili Iraq kwa lengo la kuratibu mpango wa kuwashambulia Wamarekani na kambi zao na kwamba shambulio la anga la Marekani pia lilikuwa jibu kwa hatua hizo. Hata hivyo, viongozi wa ngazi ya juu wa Iraq wamekanusha kabisa madai hayo. Adel Abdulmahdi, Waziri Mkuu wa wakati huo wa Iraq Jumapili tarehe tano Januari mwaka huu alitangaza katika bunge la nchi hiyo kuwa Kamanda Soleimani aliwasili Baghdad kwa ajili ya kupeleka ujumbe wa amani wa Iran kwa Saudi Arabia kupitia Iraq.
Abdulmahdi alisisitiza katika hotuba yake bungeni kuwa, Kamanda Soleimani alikuwa amebeba jibu la Iran kwa barua ya Saudi Arabia ambayo awali Baghdad iliiwasilisha kwa Tehran.
Tunapozingatia hayo tutaona kuwa madai ya uwongo ya Washington yamebainika wazi. Ni dhahir shahir kuwa serikali ya Trump kwa karibu mwaka mmoja na nusu uliopita ilikuwa na lengo la kumuuwa kigaidi Kamanda Soleimani; na ilikuwa tu ikitafuta fursa ya kufanya jinai hiyo. Kwa mtazamo wa washauri wa kijeshi na kiusalama wa Trump, kuwepo kwa wakati mmoja Kamanda Soleimani na Abu Mahdi al Muhandes huko Baghdad wakiwa makamanda wawili muhimu wa Iran na Iraq ilikuwa ni kikwazo kwa njama za Marekani za kuendelea kuwasaidia magaidi wa Daesh. Makamanda hao wawili wa Iran na Iraq walikuwa ni vigingi vikuu vya kufikiwa malengo haramu ya Marekani katika eneo la Asia ya Magharibi. Ndio maana serikali yenyewe ya Donald Trump huko Marekani ikawa inasema kwamba isingeliiacha fursa hiyo kupita vivi hivi hata kama makamanda hao walikuweko uraiani na si katika medani ya vita.
Ikumbukwe kuwa si George W. Bush wala Barack Obama, marais wa zamani wa Marekani aliyekuwa na uthubutu wa kufanya jinai kama hiyo. Lakini Trump yeye anajifanya ni mtu asiyetabirika katika maamuzi yake ndio maana alitoa amri ya kufanya jinai hiyo pasina kutilia maanani taathira zake. Eliot Engel, Mkuu wa Kamati ya Masuala ya Nje wa Bunge la Wawakilishi la Marekani anaamini kuwa, uamuzi wa kumuuwa kigaidi Kamanda Qassem Soleimani umezidisha mvutano kati ya Marekani na Iran na kuiweka Marekani katika mazingira hatari sana ya kuingia vitani na Iran; suala ambalo ni kwa madhara ya Marekani na wala si jambo linalopendwa na raia wa nchi hiyo.
Matamshi ya kukinzana ya White House na Trump kuhusu kuuliwa kigaidi Kamanda Soleimani akiwa pamoja na wanajihadi wenzake tisa yaliyofichuliwa na mwakilishi wa ngazi ya juu wa Baraza la Kongresi ya Marekani yanaonyesha namna Trump asivyoona aibu za kusema uongo wa aina yoyote ile alimradi tu ahalalishe jinai zake.
Post a Comment