Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amepokea taarifa ya miradi ya maendeleo ya Taasisi za Wizara yake, na kuwataka Watendaji Wakuu wa Taasisi hizo waendelea kuchapa kazi kwa kasi kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Akizungumza katika ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo jijini Dodoma, leo, Simbachawene amewataka watendaji hao kuiendeleza miradi mbalimbali iliyopo sehemu mbalimbali nchini, kwa kufanya kazi kwa kasi na ushirikiano zaidi.
“Taarifa zenu za miradi nimeisikiliza na pia mnafanya kazi vizuri, lakini lazima muisimamie miradi hiyo kwa kushirikiana kwa umoja wenu ili kufanikisha miradi hiyo iweze kusonga mbele zaidi, “ alisema Simbachawene.
Taasisi za Wizara hiyo zilizoshiriki kikao hicho ni Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uokoaji, Idara ya Uhamiaji na Makao Makuu ya Wizara hiyo, ambazo kila Taasisi ziliwasilisha taarifa zake katika kikao hicho, na kujadiliana hatua iliyofikia miradi hiyo, changomoto zilizopo, pamoja na kuzitafutia suluhisho.
Pia kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Christopher Kadio, Naibu Katibu Mkuu, Ramadhani Kailima, na viongozi hao waliweza kusikiliza miradi hiyo kwa ufasaha na kutoa njia za kuifanikisha zaidi kwa kuiendeleza miradi hiyo.
Baadhi ya miradi iliyowasilishwa katika kikao hicho, upande wa Polisi;, ujenzi wa jengo la Makao Makuu Dodoma, ujenzi wa Kituo cha Polisi Ludewa Mkoani Njombe, ujenzi wa Jengo la Polisi Mkoa wa Manyara, na upande wa Idara ya Uhamiaji;- ujenzi wa Jengo la Makao Makuu Dodoma, na upande wa Zimamoto;, Ujenzi wa jengo la Makao Makuu Dodoma.
Kwa upande wa miradi ya Magereza; ujenzi wa Gereza Ruangwa Mkoani Lindi, Igunga na Urambo Mahabusu-Tabora, Mradi wa Umwagiliaji Gereza Idete-Morogoro na Gereza Kitengule-Kagera, na Ujenzi wa Kiwanda cha Seremala Msalato-Dodoma, ujenzi wa Kiwanda cha Viatu Gereza Karanga, na ujenzi wa Kiwanda cha Sukari Gereza Mbigiri-Morogoro.
Waziri Simbachawene, wiki iliyopita alikabidhiwa ofisi na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, Kangi Lugola, na baada ya makabidhio hayo, aliwataka viongozi wa Wizara hiyo na Taasisi zake, wafanye kazi usiku na mchana ili nchi iweze kusonga mbele.
Alisema kwasasa Tanzania katika Afrika inaonekana watu wake wanajenga nchi kwa kasi, hivyo heshima hiyo imeletwa na Rais John Magufuli, hivyo Watanzania wanapasawa kuwa mashabiki wake kwa kuunga mkono juhudi hizo yenye nia ya kuiendeleza nchi.
Post a Comment