Featured

    Featured Posts

IMF YAIPONGEZA TANZANIA KWA KUBORESHA MAZINGIRA YA KIBIASHARA NA KUDHIBITI MFUMUKO WA BEI

Charles James, Michuzi TV

TANZANIA imepongezwa na Shirika la Fedha duniani (IMF) kutokana na namna ilivyoboresha mazingira ya kibiashara, kudhibiti mfumuko wa bei ambao uko chini ya asilimia tano, ongezeko la mikopo sekta binafsi pamoja na uimara wa kuwa na fedha nyingi za kigeni kulinganisha na Nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Ripoti ya Shirika hilo iliyotolewa Machi mwaka inaeleza kuridhishwa na deni la Taifa ambalo wamelitaja kuwa himilivu na linaifanya Tanzania iendelee kupokea mikopo kwani wamekua wakikopa na kulipa vizuri.

Akizungumza na wandishi wa habari leo jijini Dodoma, Msemaji Mkuu wa Serikali Dk Hassan Abbas amesema shirika hilo poa limevutiwa na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi yanayofanywa na serikali bila kumuonea mtu.

" Wote tunaona namna Rais Magufuli alivyo mstari wa mbele katika vita dhidi ya rushwa na kusimamia sheria, wenzetu wameona hayo na wametupongeza sana. Lakini pia wamefurahishwa na makusanyo ya kodi ambayo kwa miaka hii minne tumepiga hatua kubwa sana.

Pamoja na kutupongeza wametushauri mambo mbalimbali ambayo mengine mengi tumeshaanza kuyafanya. Ambapo sasa tunakuja na mkakati unaoitwa Blue Print wenye lengo la kuboresha mazingira ya kibiashara nchini," Amesema Dk Abbas.

IMF pia wametambua na kusifu juhudi za serikali katika kusimamia na kuwekeza katika sekta ya afya huku pia wakishauri serikali kuendelea kuwekeza kwenye sekta ya miundombinu.

Akizungumzia mafanikio ya serikali ya awamu ya tano kwenye sekta ya ardhi, Dk Abbas amesema hapana shaka serikali imefanya kazi kubwa ya kumaliza migogoro ya muda mrefu ya ardhi iliyokua ikiwafanya wananchi wakose furaha.

Amesema Machi 4, mwaka huu serikali kwa maana ya Wizara ya Ardhi ilitatua na kumaliza kero zaidi ya 10,000 ambapo pia vijiji 900 vilivyokua vimeingiliwa na hifadhi vilitengwa bila kunyang'anywa ardhi yake.

" Hatutaki kuona watanzania wakinyanyasika au wakijuta kumiliki ardhi hivyo ni jukumu la serikali kutatua changamoto zilizopo kwenye ardhi lakini pia kutoa elimu kwa watu wetu itakayofanya wajue pia umuhimu wa kuwa na hati.

Kupitia utatuzi wa migogoro hiyo serikali imepata ongezeko la mapato mengi yatokanayo na ardhi ambapo ndani ya miaka minne mapato yameongezeka kutoka Sh Bilioni 54 kwa mwaka 2015 hadi Sh Bilioni 100 kwa takwimu za mwaka jana, mwaka huu yatakua juu zaidi," Amesema Dk Abbas.

SEKTA YA MAJI

Katika kuendelea kuhudumia wananchi serikali pia imeendelea kutekeleza kwa kasi miradi ya maji ambapo sasa imefikia asilimia 85 kwa Mijini na asilimia 64 kwa vijijini huku malengo yakiwa kufikia asilimia 95 kwa mijini na 85 kwa vijijini kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Dk Abbas amesema tayari mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Viktoria unaomwaga maji katika maeneo ya Mkoa wa Shinyanga na zaidi Mkoa wa Tabora umeshakamilika na sasa wananchi wa Igunga, Nzega na maeneo mengine ya Tabora wanatumia maji ya Ziwa Viktoria.

Amesema mradi huo umetumia takribani Sh Bilioni 600 na utahudumia vijiji zaidi ya 90 na watu zaidi ya Milioni Moja watanufaika na mradi huo katika maeneo yote ya Mkoa wa Tabora.

UWANJA WA NDEGE MSALATO

Kuhusu ujenzi wa uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma, Dk Abbas amesema tayari fedha za mradi huo mkubwa zimeshapatikana na kwamba wananchi wa Mkoa wa Dodoma wakae tayari kwa ajili ya kushuhudia kuanza kwa ujenzi huo.

" Serikali ya awamu ya tano chini ya Dk John Magufuli inaahidi na kutenda, tayari kiasi cha Dola Milioni 271 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo wa kisasa zishapatikana, michoro ya ramani ishakua tayari kilichobaki ni ujenzi kuanza mara moja, hii ni kuonesha kweli tumedhamiria kutekeleza kilichoahidiwa," Amesema Dk Abbas..
Msemaji Mkuu wa Serikali Dk Hassan Abbas akizungumza na wandishi wa habari kuhusiana na mambo mbalimbali yanayohusu Nchi yetu leo hii jijini Dodoma.
 Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbas akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma leo.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana