Rais Dk. John Magufuli akisalimiana na Mwanasiasa Mkongwe ambaye ni Mwanachama wa Chama cha ACT- Wazalendo Maalim Seif Sharif Hamad kwa kutokugusana mikono, Ikulu Jijini Dar es Salaam, leo. Salamu hiyo ya kutokugusana mikono ni kutekeleza ushauri ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wenye lengo kujihadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona. PICHA ZAIDI> BOFYA HAPA
IKULU, Dar es Salaam
Rais Dk. John Magufuli amefanya mazungumzo na wanasiasa, Maalim Seif Sharif Hamad, Prof. Ibrahimu Lipumba na James Mbatia, Ikulu Jijini Dar es Salaam, leo.
Baada ya mazungumzo hayo, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mstaafu amesema yeye na Mhe. Rais Magufuli wamezungumzia masuala ya kudumisha amani, usalama na upendo kwa watu wote, na ameelezea kufurahishwa kwake na dhamira ya Rais Magufuli kukutana na viongozi mbalimbali na kujadiliana mambo yenye maslahi kwa nchi.
Kwa upande wake, Prof. Ibrahim Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) amempongeza Rais Magufuli kwa ahadi yake kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu (2020) utakuwa huru na wa haki na amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kupambana na rushwa, kudhibiti matumizi ya Serikali, kulinda na kutumia vizuri rasilimali za Taifa, kuboresha elimu na kuimarisha uchumi.
Prof. Lipumba ametoa wito kwa Watanzania wote kuweka uzalendo mbele, kudumisha amani na utawala bora, na amewataka wanachama wote wa CUF kujiandaa kushiriki Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu kwa kufuata taratibu na sheria zilizopo.
Prof. Lipumba amewakosoa wanasiasa wanaopinga kila jambo linalofanywa na Serikali na amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano (iliyo chini ya Chama Cha Mapinduzi – CCM) imetekeleza vizuri mambo mengi yaliyokuwa yakisemwa na vyama vya upinzani, hivyo sio sawa kwa vyama hivyo kupinga jambo vililotaka litekelezwe na linatekelezwa, mfano kurekebisha sheria ya madini na kupambana na rushwa.
Kwa upande wake James Francis Mbatia pamoja na kufurahishwa na dhamira ya Rais Magufuli juu ya Uchaguzi Mkuu kuwa huru na wa haki ametaka wanasiasa waache kukamiana na kuchochea mambo hasi dhidi ya Taifa, na badala yake waungane kuendeleza mambo mazuri yanayofanywa na Serikali ikiwemo kuboresha elimu, upatikanaji wa nishati na mengine yenye maslahi mapana kwa wananchi.
Mbatia ametoa wito kwa wanasiasa na Watanzania wote kwa ujumla kuweka mbele maslahi ya Taifa badala ya kukumbatia mambo yenye maslahi binafsi, na ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kufanya vizuri katika maeneo mbalimbali licha ya kwamba wapo baadhi ya watu wanaobeza mafanikio hayo.
Post a Comment