Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme, amemtaka wakala wa usajili ufilisi na udhamini (RITA) na wakuu wa wilaya zinazopakana na Nchi jirani kuhakikisha wanawadhibiti watoto walio na umri chini ya miaka mitano ambao sio raia wa Tanzania kuingizwa kwenye mpango wa usajili wa vizazi utakaoanza mapema mwaka huu.
Mndeme alitoa rai hiyo jana wakati alipokuwa akifungua warsha ya viongozi wa wilaya na mkoa wa Ruvuma kuhusu usajili wa vizazi kwa watoto wa umri wa chini ya miaka mitano iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa manispaa ya Songea mkoani humo.
Alisema kuna baadhi ya wilaya mkoani humo zinapakana na Nchi jirani za Msumbiji na Malawi hivyo katika kukabiliana na changamoto hiyo ameviomba vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha watoto hao wasio na sifa hawasajiliwi katika mpango huo na kwamba watakaosajiliwa ni wale waliokidhi vigezo.
Aidha mkuu huyo wa mkoa wa Ruvuma Mndeme,amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawasajili watoto wao pindi wanapozaliwa kwa lengo la kuiwezesha serikali kuwa na takwimu sahihi ili iweze kupanga mipango ya maendeleo ya muda mfupi na mrefu kwa madai kwamba bila ya kufanya hivyo itakuwa vigumu kuweza kujua mahitaji halisi kwa ya wananchi.
“Nawaombeni wasajili kwenye vituo vya tiba na watendaji wa kata mtangulize uzalendo na uadilifu katika mpango huo kwa lengo la kuepuka urasimu utakaosababisha wananchi kutozwa fedha hivyo yeyote atakayekwenda kinyume na utaratibu atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sharia”Alisema Mndeme
Hata hivyo Mndeme ameonyesha kutoridhishwa na takwimu za sense ya watu na makazi ya mwaka 2012 ambayo inaonesha ni asilimia 6 pekee ya watoto wa mkoa wa Ruvuma ndio waliosajiliwa nakupatiwa vyeti vya kuzaliwa ambapo amedai kwamba kwa ujumla takwimu hizo hazirizishi na haziwezi kusaidia kupanga mipango ya maendeleo.
Awali kaimu Afisa mtendaji mkuu wa RITA Emmy Hudson alisema kuwa lengo la warsha hiyo ni kutoa hamasa kwa ajili ya usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano kwa madai kwamba mpaka sasa kiwango cha watoto waliosajiliwa ni kidogo.
Hudson aliongeza kusema kuwa mpaka sasa watoto walio na umri chini ya miaka mitano waliosajiliwa hapa Nchini ni zaidi ya milioni nne na kwamba katika kuboresha mpango huo wameamua kusogeza huduma hiyo kwa lengo la kuwapunguzia adha yaufuatiliaji na kuwapunguzia gharama.
Kaimu Afisa mtendaji huyo mkuu wa RITA Hudson aliendelea kusema kuwa katika kuboresha mpango huo,huduma zitakuwa zinapatikana katika ofisi zote za watendaji kata na vituo vya Tiba vinavyotoa huduma ya mama na mtoto.
Warsha hiyo imeshirikisha viongozi mbalimbali wakiwemo wakuu wa wilaya,wenyeviti wa Halmashauri,wakurugenzi wa Halmashauri,makatibu tawala,makatibu tawala wasaidizi,viongozi wa Dini na wawakilishi wa wadau wa maendeleo wakiwemo UNICEF.
Post a Comment