Featured

    Featured Posts

SERIKALI YAFUNGA SHULE ZA AWALI HADI KIDATO CHA SITA KWA SIKU 30 KUIHAMI NCHI NA CORONA, YAFUNGA PIA MIKUSANYIKO YA SIASA NA MICHEZO



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana kuhusu hatua za awali zilizochukuliwa na Serikali kutokana na kuwepo nchini virusi vya ugonjwa wa Corona. 






DAR ES SALAAM, Tanzania
Serikali imezifunga shule za awali hadi kidato cha sita kwa siku 30 na pia kuzuia mikusanyiko yoyote ikiwemo ya siasa na michezo ili kuihami nchi na ugonjwa wa Corona ambao umethibishwa kuingia nchini kufuatia kupatikana kwa mgonjwa mmoja wa ugonjwa huo hapa nchini.

Hatua hizo zimetangazwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akitoa msimamo wa Serikali kupitia vyombo vya habari kuhusiana ugonjwa huo, leo jijini Dar es Salaam.

 “Tumefunga shule zote kuanzia za awali hadi kidato cha sita, tumesitisha michezo yote ikiwemo ligi kuu na Serikali imefikia uamuzi huo ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo nchini” alisema Waziri Mkuu.

Alisema, Serikali inaendelea kuchukua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzuia mikusanyiko yote ambayo si ya lazima kufanyika kama vile semina na shughuli mbalimbali za kijamii.

Waziri Mkuu Majaliwa, alisema kuwa Serikali imeendelea kufuatilia abiria wanaoingia nchini kupitia maeneo ya viwanja vya ndege na mipakani, kwa kuwapima abiria ili kubaini kama wanamaambukizi, sambamba na kuimarisha maabara ili iweze kupima na kutambua endapo kuna maambukizi.

“Tumetenga kambi maalum eneo la Mloganzila jijini Dar es Salaam, Kituo cha afya cha Buswelo jijini Mwanza, Hospitali ya Mawenzi mkoani Kilimanjaro na Hospitali za Mnazi mmoja, Zanzibar na Chakechake Pemba, ambazo zitatumika kuhudumia wagonjwa wa Corona”, alisema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu alisema, jitihada nyingine zilizofanywa na Serikali ni kusitisha shughuli za Mwenge na badala yake fedha hizo Sh. Bilioni moja ambazo zingetumika kwenye shughuli hizo za Mwenge kuwashwa na kukimbizwa zimeelekezwa Wizara ya Afya ili kuwezesha shughuli mbalimbali zitakazosaidia kupambana na ugonjwa huo na tayari Sh. milioni 500 zimeshakabidhiwa Wizara ya Afya.

“Wizara ya Afya ihakikishe vifaa vya kinga ikiwemo vimiminika vya kuthibiti maambukizi (hand sanitizer) vinapatikana katika maduka yote husika na kwa bei ya kawaida na Serikali itachukua hatua kwa wafanyabiashara watakaobainika kufanya ulanguzi wa viaa hivyo.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kote nchini kufuatilia kwa karibu na kufanya uchunguzi kuhusu wageni watakao ingia katika maeneo yao, na wananchi wametakiwa kutoa taarifa katika namba za bure za 0800110037/0800110124 na 0800110125 pindi watakapohisi kuwa na dalili za ugonjwa wa Corona ili Serikali iweze kuchukua hatua za haraka.

Ugonjwa wa Corona ulioanza Disemba mwaka jana nchini China, umesambaa  zaidi katika nchi 150 Duniani, na mgonjwa wa kwanza amepatikana hapa nchini, jana, Machi 16 mwaka huu, ambaye aliwasili nchini kutoka Ubelgiji.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana