Na Bahati Mollel,TAA
BODI ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imeiangukia serikali iisaidie TAA kuigharama huduma mbalimbali za uendeshaji kwenye viwanja vya ndege kutokana na kuathiriwa kwa asilimia 100 na ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID19), inayoambukizwa na virusi vya corona.
Mwenyekiti wa MAB, Dkt. Masatu Chiguma, ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki kwenye kikao cha dharura cha Bodi hiyo, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jengo la Watu Mashuhuri lililopo katika Jengo la Pili la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (VIP-TB2-JNIA.
Dkt. Chiguma amesema ugonjwa huu ambao upo nchini ulianzia nchini China mwishoni mwa mwaka 2019 na tarehe 11 Machi, 2020 Shirika la Afya Duniani (WHO), kuutangaza rasmi kuwa ni janga lililoikumba dunia nzima, baada ya kusambaa kwenye nchi kadhaa na wananchi wake kupata maambukizi na wengine kupoteza maisha. Tanzania hadi sasa ina maambukizi 147 na waliofariki ni watano.
“Imetulazimu kuitisha kikao hiki cha dharura haraka ili kupata tathmini ya madhara yaliyoikumba TAA kutokana na huu ugonjwa wa COVID19 baada ya kusimamishwa kwa ndege za abiria za nje ya nchi kuingia nchini. Hii ni kuzingatia kuwa asilimia 70 ya bajeti ya TAA inatokana na makusanyo yake ya ndani yanayotokana tozo mbali mbali za kuhudumia ndege na abiria viwanjani na asilimia 30 inatolewa na Serikali. Aidha TAA ni mmoja ya taasis za umma zinazotoa changia vizuri pato la taifa” alisema Dkt Chiguma.
Amesema ugonjwa huu umeathiri hata safari za ndege zinazofanywa ndani ambazo zimeshuka kwa asilimia 40, ambapo kwa ndege za Shirika la ndege la Tanzania (ATCL), Precision Air, Coastal Aviation, Auric na nyingine zimepungua safari zao kutokana na kupungua au kutokuwepo kwa abiria wanaotoka nje ya nchi waliokuwa wakisafiri kwenda mikoa mbalimbali yenye vivutio vya asili.
Dkt. Chiguma amesema bado ugonjwa huu upo nchini, hivyo wanatarajia kuwasilisha rasmi maombi serikalini ya kuisaidia TAA iendelee kuhudumia viwanja vyetu kulingana na viwango vya kimataifa vinavyotakiwa.
Hatahivyo, ameipongeza menejimenti ya TAA, kuchukua hatua za haraka za kwa kufuta baadhi ya matumizi yasiyo ya lazima kwa kuzingatia miruko ya ndege imepungua na maelekezo ya Serikali ya kupambana na ugonjwa wa COVID 19 na kuzielekeza kwa utunzaji na uendeshaji wa viwanja vya ndege na mapambano dhidi ya virusi vya CORONA
Awali Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mhandisi Mshauri Julius Ndyamukama aliiambia MAB kuwa baada ya kusitishwa kwa safari za ndege za nje ya nchi na hata baadhi ya ndege za ndani kupunguza miruko yake kwa asilimia 40, kutasababisha Mamlaka kukabiliwa uhaba mkubwa wa fedha za uendeshaji wa shughuli mbalimbali na kufanya zishindwe kufanyika kwa wakati, kutokana na kutegemea mapato yatokanayo na ada za kutua na kuruka kwa ndege, maegesho ya ndege, tozo za abiria, pango na maegesho ya magari.
Amesema hadi sasa TAA imepoteza mapato makubwa ya zaidi ya asilimia 64.7 kwa kuwa wanategemea zaidi Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), ambacho kinatumiwa asilimia 43 ya abiria wote Tanzania na asilimia 40 ya Watalii wanaotoka nje ya nchi wanatumia kiwanja hiki. Kwa kuonyesha jinsi hali ilivyo kwa sasa alisema mwezi Februari JNIA ilihudumia miruko ya ndege za nje 158, hapa nchini (domestic) 167 na ndogo ndogo (general aviation) 465; ambapo kwa mwezi Machi kabla ya kusitishwa kwa ndege za nje ya nchi abiria kutoka nje ya nchi walipungua kwa asilimia 95 na wa ndani ya nchi walipungua kwa kiasi cha asilimia 60.
Aidha katika utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kupambana na virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID 19) TAA imehakikisha wafanyakazi na wadau wake waliopo katika mazingira ya viwanja wanafuata maelekezo ya kutaka kila mmoja anachukua hatua ya kujikinga ikiwa na kuepuka mikusanyiko, kutumia zaidi simu za mezani, mawasiliano ya kieletroniki, kunawa mikono mara kwa mara kwa kutumia maji tiririka na yenye dawa ya chlorine, pia kumewekwa mabango yenye ujumbe wa namna ya kujikinga maeneo mbalimbali, pia TAA wamenunua vifaa tiba kwa ajili ya watumishi wake zikiwemo barakoa, vitakasa mikono na kipimia joto la mwili (thermostats), ambapo kabla ya kuingia ofisini wanapimwa. Tunamshukuru Mungu hadi sasa hatuna Mtumishi aliyeathirika na ugonjwa huu.
Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Paul Rwegasha mwishoni mwa wiki akitakasa mikono ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu (COVID19), wakati alipoingia kwenye Jengo la Watu Mashuhuri (VIP), kushiriki kwenye kikao cha dharura cha Bodi ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).
Mjumbe wa Bodi ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Dkt. Paschal Mugabe (kulia), akipimwa joto la mwili na Afisa Afya Bi. Zaina Yassin kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto mwishoni mwa wiki alipoudhuria kikao cha dharura kilichofanyika kwenye Jengo la Watu Mashuhuri la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mazingira cha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Maxmilian Mahangila (mwenye koti jeupe kushoto), mwishoni mwa wiki akiwasilisha kwa Bodi ya Ushauri (MAB) ya TAA, ripoti ya madhara ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID19) unaoambukizwa na virusi vya corona kwa upande wa uendeshaji wa viwanja vya ndege
Wajumbe wa Bodi ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wakimsikiliza Meneja wa Mipango na Takwimu wa Mamlaka hiyo, Bi. Asteria Mushi (wa kwanza kushoto) akiwasilisha ripoti ya madhara ya COVID 19 ikiwemo ya kusitishwa kwa ndege za nje ya nchi na kupunguza miruko ya ndege za ndani kulivyoathiri mapato ya mamlaka hiyo yanayotokana na ada na tozo mbalimbali.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri (MAB), ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Dkt Masatu Chiguma (wa kwanza kulia), akizungumza jambo kwenye kikao cha dharura kilichofanyika mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi wa mikutano wa Jengo la Watu Mashuhuri la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), kilichojadili madhara ya awali yaliyosababishwa na ugonjwa wa homa kali ya Mapafu (COVID19) inayoambukizwa na virusi vya corona.
Post a Comment